Pigo Tena Upinzani: Wanachama Wengine 1,200 wa Chadema Watimkia CCM
Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimezidi kumomonyoka baada ya
wanachama wao zaidi 1,200, wakiwemo viongozi wakuu wa Wilaya ya
Ngorongoro, kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Miongoni mwa viongozi waliohama ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti
wa Chadema wa Wilaya Ngorongoro, Samweli Ole Nakumbale, aliyekuwa
mgombea ubunge wa jimbo hilo mwaka 2015, Elias Ngorisa na aliyekuwa
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVITA) Wilaya ya Ngorongoro, Wiliam ole
Telele.
Wakizungumza baada ya kuomba kurudi CCM na kupokewa wakati wa
uzinduzi wa kampeni za CCM za ubunge katika Jimbo la Longido juzi,
walisema kuwa ubinafsi ndani ya Chadema umekithiri na vyeo katika chama
hicho hutolewa kwa kuangalia sura na ukabila.
“Nilikuwa kada wa CCM nikachukuliwa na mafuriko ya mwaka 2015
nimekaa huko hakuna kipya ni usanii mtupu. Chama hakina hata ofisi ya
wilaya kwenye baadhi ya mikoa lakini baada ya kulinganisha nikaona kweli
nimepotea njia,” alisema Nakumbale.
Naye Ngorisa alisema mwanaume mwenye busara, ni yule
anayejitafakari na kujitathimini katika maamuzi yake. “Nimekaa
nimetafakari kwa kina, nikaona kweli kuna mahali nilikosea na ndiyo
maana nikaamua kurudi CCM, kwa kuwa ilani yake inatekelezeka kwa vitendo
na wananchi wanafurahia utendaji wa Rais John Magufuli”.
Alisema kibaya zaidi amekuwa akiandikwa vibaya kila siku kwenye
mitandao ya kijamii kwa mambo ya uongo na uzushi yasiyokuwa na tija,
hali ambayo imemfanya arudi CCM.
“Nimetuhumiwa sana kwenye mitandao nikiitwa msaliti wakati si
kweli, lakini sasa kutokana na tuhuma zao ambazo hazikuwa na mashiko
nimeamua kurudi CCM.
“Nimekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa
miaka 10 kupitia CCM na ukweli kuna mahali tulikosea baadhi ya viongozi,
tulikuwa na maslahi binafsi badala ya kuhangaika na kero za wananchi,
lakini Mungu ametupa Rais mzalendo aliyejitoa sadaka kwa ajili ya
kupambana na mafisadi na kusimamia rasilimali za nchi,” alisema.
Kwa upande wake, mfanyabiashara maarufu katika Wilaya ya Longido
ambaye pia ni Laigwanani wa mila ya jamii ya Kimasai, Eliya Malari
alisema wazee wa mila walilala kwake siku 10 wakimuomba arudi CCM, na
baada ya kutafakari utendaji wa Rais Magufuli, alikubali ombi la wazee
hao na kuamua kurudi CCM na wafuasi wake
No comments:
Post a Comment