Afrika Imeamua.....Marais Afrika Nzima Kukutana January Kwa Ajili ya Mageuzi Makubwa
Wakuu
wa nchi na Serikali za Afrika, wakiwemo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), mapema mwakani wanatarajiwa kusaini makubaliano ya kuanzishwa kwa
eneo huru la biashara la bara hilo (CFTA).
Wanatarajiwa
kuwa na mkutano wa 30 wa kawaida Januari 28 na 29 mwakani katika ukumbi
wa Nelson Mandela uliopo kwenye Kituo kipya cha Mikutano (AUC) jijini
Addis Ababa, Ethiopia.
Mkutano
huo utakaokuwa nakaulimbiu; “Kushinda Vita Dhidi ya Rushwa: Mwelekeo
Endelevu wa Mabadiliko Afrika,” utatanguliwa na mkutano wa 35 wa Kamati
ya Wawakilishi wa Kudumu (Januari 22-23) na mkutano wa 32 wa kawaida wa
Baraza la Utendaji (Januari 25-26).
CFTA
itakuwa soko la zaidi ya watu bilioni 1.3 na wanatarajiwa kufika
takribani bilioni mbili ifikapo mwaka 2025. Yatakaposainiwa, makubaliano
hayo ya kibiashara yatakuwa makubwa zaidi barani humo yakizihusu nchi
zote 54 za Afrika, na yatakuwa ya pili kwa ukubwa duniani. Makubaliano
makubwa zaidi duniani ni ya Shirika la Biashara la Dunia (WTO)
yaliyosainiwa mwaka 1994.
Kwa
sasa Afrika ina masoko mawili makubwa yanayozihusu baadhi ya nchi,
ikiwemo Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Soko la
Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).
EAC
yenye nchi sita wanachama za Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini,
Tanzania na Kenya, ina zaidi ya watu milioni 170. Mkutano wa 18 wa
kawaida wa wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika
Addis Ababa, Ethiopia Januari 2012, uliamua kuwa hadi mwaka 2017 CFTA
iwe imeanzishwa. Majadiliano kuhusu uanzishwaji huo yalianza rasmi Juni
2015.
Juni
mwaka huohuo, wakati wa mkutano wa 25 wa wakuu wa nchi za AU
uliofanyika Afrika Kusini, viongozi hao walikubaliana lianzishwe eneo
huru la biashara ifikapo mwaka 2017 kupitia makubaliano na biashara
huria za bidhaa na huduma.
Kwenye
mkutano wa nne wa mawaziri wa biashara kutoka nchi za Afrika,
uliofanyika hivi karibuni Niamey, Niger viongozi hao waliidhinisha
muundo wa makubaliano na kuzingatia maendeleo, yaliyofikiwa kwenye
majadiliano ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano ujao wa wakuu wa
nchi na serikali. CFTA itatoa uhakika wa mazingira ya uwekezaji,
maendeleo ya viwanda na ongezeko la thamani ya bidhaa na huduma, hivyo
kutengeneza fursa za ajira na vipato vya familia.
Hivi
karibuni, wakati anafungua mkutano wa mawaziri mjini Niamey, Rais wa
Jamhuri ya Niger Issoufou Mahamadou alipongeza maendeleo yaliyofikiwa
katika majadiliano kuhusu makubaliano hayo.
CFTA
na makubaliano mengine yakiwemo ya Kuharakisha Maendeleo ya Viwanda
Afrika (AIDA), Programu ya Maendeleo ya Kilimo Afrika (CAADP), Mpango wa
Programu ya Maendeleo ya Miundombinu Afrika (PIDA) vitaiwezesha Afrika
kufanikiwa katika malengo ya mabadiliko.
Makubaliano
ya kuanzisha eneo huru la biashara Afrika, yanaweka ajenda kwa ajili ya
mijadala kuhusu biashara ya bidhaa, biashara ya huduma na utatuzi wa
migogoro. CFTA itashughulikia itifaki mbili, ikiwemo ya biashara ya
bidhaa na itifaki ya biashara ya huduma. Makubaliano hayo yanatarajiwa
kuboresha biashara baina ya nchi za Afrika.
Malengo
makuu ya CFTA ni kuiwezesha Afrika kuwa na soko moja la bidhaa na
huduma, litakalotoa uhuru kwa wafanyabiashara na uwekezaji na hivyo
kutoa fursa ya kuongeza kasi ya kuanzisha umoja wa forodha barani humu.
No comments:
Post a Comment