Trending News>>

CUF Lipumba Yagonga Mwamba Tena Mahakamani

Maombi ya kumtaka Jaji  Wilfred Ndyansobera ajitoe katika kusikiliza mashauri ya Chama cha Wananchi (CUF) yanayoendelea katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, yamekataliwa na kutupiliwa mbali.

Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na watu 10 wanaodaiwa kuwa ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini CUF ya Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, ambapo barua ya maombi hayo ilikuwa na malalamiko sita ikiwemo wadaiwa kutokuwa na imani na jaji.

Akisoma maamuzi ya kutokujitoa kusikiliza mashauri hayo leo Novemba 13, 2017, mbele ya mahakama, Jaji Ndyansobera, amedai kuwa baada ya kuchunguza malalamiko hayo, na kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili, amegundua kuwa hakuna kitu kinachoonyesha kama anapendelea upande mmoja, pia malalamiko hayo yalikuwa si sahihi kisheria kutokana kwamba watu 10 waliowasilisha maombi hayo, ni watu binafsi na si bodi halali ya wadhamini ya CUF.

“Bodi ya CUF ina taratibu zake za kutekeleza majukumu yake, mtu hawezi kusema anatumwa na bodi, bali bodi hufanya kazi zake. Jaji kujiondoa sio kitu chepesi ni kitu kizito,” amesema Ndyannsobera.

Jaji Ndyansobera amedai kuwa, katika kusikiliza mashauri ya CUF, alifuata sheria na katiba ya nchi, ambapo sheria inamtaka jaji kutekeleza majukumu yake katika kutoa haki, bila ya woga wala upendeleo au shinikizo kutoka upande wowote.

“Kuna mambo mawili ya msingi ya kuzingatia, jaji anatakiwa kujiondoa kwa kuzingatia mazingira ya kesi kama alikuwa anapendelea… pili kama kuna uhusiano wa karibu na mtu mmojawapo kwenye kesi au masilahi binafsi, jaji inatakiwa ujiondoe. Mahakama inatakiwa kuwa huru, jaji au Mahakama inaweza kuamua kesi kwa kuzingatia ushahidi ulioko mbele yake pasipo kupata mashinikizo kutoka nje na ubaguzi,” ameongeza.

Hali kadhalika ametaja sababu tano zilizopelekea kutokujitoa katika kusikiliza mashauri hayo, ikiwemo kuzuia ucheleweshwaji wa kesi, upotevu wa fedha, pia Jaji aliyekuwepo (Ndyansobera) ameshatoa maamuzi kwenye baadhi ya kesi hivyo inabidi aendelee kusikiliza mashauri kutokana kwamba anazijua kesi vizuri.

No comments:

Powered by Blogger.