Trending News>>

KUFELI KWA FIGO (KIDNEY FAILURE)


KUFELI kwa figo, ni hali ambayo hutokea taratibu na ni vigumu kwa mtu wa kawaida kujua kwamba figo zake zinaelekea kufeli. Yapo mambo mengi yanayoweza kusababisha figo ikafeli, yakiwemo magonjwa kama kisukari, shinikizo la juu la damu, kutumia dawa kali kwa kipindi kirefu, kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua au kwenye ajali, kutumia dozi kubwa za madawa ya kulevya nk.
Mgonjwa anapofikia hatua ya figo yake kufeli, ni lazima kilichosababisha akafikia hatua hiyo kishughulikiwe mapema ambapo akipata matibabu sahihi kwa muda muafaka, figo zinaweza kurudi
kufanya kazi kama zamani (kwa baadhi ya watu). Matibabu hayo ni pamoja na kuanzishiwa tiba ya kusafisha damu kwa kutumia mashine inayofanya kazi sawa na figo (dialysis). Inaposhindikana, hakuna njia nyingine ya kumsaidia mgonjwa zaidi ya kupandikizwa figo nyingine (kidney transplant) ingawa zipo pia tiba mbadala ambazo mgonjwa hata kama hospitalini matibabu yameshindikana, anaweza kutibiwa na akapona bila kupandikizwa figo nyingine, hatua ambayo huwa ya mwisho kabisa. Zipo dalili nyingi zinazoweza kukuonesha kwamba figo zako zina matatizo.
Dalili hizo ni pamoja na; kupungua sana kwa kiwango cha mkojo au kukojoa sana hasa
nyakati za usiku, kukojoa mkojo wenye povu jingi, maji kurundikana ndani ya mwili na kusababisha kuvimba kwa viungo kama miguu, uso na wengine huvimba mwili mzima.

Dalili nyingine ni mwili kuishiwa nguvu (fatigue), kichefuchefu, kusinzia mara kwa mara, kukosa pumzi, kupatwa na maradhi ya ngozi, kusikia kizunguzungu, kupoteza ladha ya chakula mdomoni, kuchanganyikiwa na kukosa uzingativu na kwa baadhi ya watu, hupatwa na tatizo la kuzimia mara kwa mara.

Unapoona moja au zaidi ya dalili zilizotajwa hapo juu, ni muhimu kuwahi hospitali ambako utapimwa na kuanza matibabu kulingana na matatizo yako. Endapo mgonjwa mwenye matatizo ya figo atawahi kwenda hospitali na kupatiwa tiba ya uhakika, atafuata masharti ya daktari na kuishi kwa kuzingatia misingi ya afya bora, mgonjwa wa figo anaweza kuishi maisha marefu kama mtu asiye na matatizo hayo.

No comments:

Powered by Blogger.