MKUU WA WILAYA YA KINONDONI, ALLY HAPI AJIVUA SAKATA LA KUKAMATWA MBUNGE HALIMA MDEE
BAADA
ya Jeshi la Polisi kumshikilia kwa zaidi ya saa 48 Mbunge wa Kawe,
Halima Mdee, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, ambaye ndiye chanzo
cha kukamatwa kwa mwanasiasa huyo, amejivua kwenye sakata hilo.
Jana
jeshi hilo lilimuhamisha Mdee kutoka katika mahabusu za Kituo cha
Oysterbay alikokaa kwa siku nne na kumpeleka Kituo Kikuu cha Polisi
(Central), ambako anaendelea kushikiliwa kwa kosa la uchochezi.
MTANZANIA
Jumapili lilipomtafuta Hapi ili kufahamu kama amri ya saa 48 alizozitoa
kwa polisi kumshikilia Mdee ina mabadiliko yoyote, alisema kwa sasa
suala hilo asiulizwe yeye bali Jeshi la Polisi.
“Muulizeni Kaimu wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,” alisema Hapi bila kufafanua.
MTANZANIA
Jumapili lilipomtafuta Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Lucas Mkondya na kumuuliza kuhusu hilo, alijibu kuwa yuko
likizo.
“Niko likizo, sijui kama (Mdee) yupo hapo, mtafute Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala,” alisema Mkondya.
Alipotafutwa
kwa simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, alikiri kuwa
ni kweli mbunge huyo alipelekwa hapo kwa mahojiano.
“Aliletwa hapa kwa mahojiano, lakini ni suala la Kanda Maalumu,” alisema Kamanda Hamduni.
Alipoulizwa msingi wa mahojiano hayo, Kamanda Hamduni alisema kuwa hilo ni suala la kipelelezi kupitia Kanda Maalumu.
“Mimi si mpelelezi, anayepeleleza ni Kanda Maalumu,” alisema.
Mdee
ambaye alihojiwa kwa saa kadhaa jana mara tu baada ya kuhamishiwa Kituo
Kikuu cha Polisi, hakupatiwa dhamana kwa kile kilichoelezwa askari
waliopewa jukumu la kumuhoji hawakuwa na maelekezo mengine.
Awali,
MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Wakili wa Mdee, Hekima Mwasipu ambaye
alifafanua kuwa mteja wake alihojiwa kwa kosa la uchochezi.
“Ni kweli alihamishiwa Kanda Maalumu leo (jana),” alisema Mwasipu.
MTANZANIA
Jumapili lilitaka kufahamu sababu za Mdee kuhamishwa kutoka Kituo cha
Oysterbay na kupelekwa Kanda Maalumu ambako ameendelea kushikiliwa licha
ya saa 48 kupita, Mwasipu alisema hata yeye alihoji na kujibiwa kuwa ni
suala la polisi kanda hiyo.
“Sababu
za kumtoa kule na kumleta Kanda Maalumu sielewi ni nini, lakini
ninachoweza kusema ni kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa
kushirikiana.
“Ila
kwa maelezo yao hata mimi nilipowahoji walijibu kwamba makosa hayo yako
chini ya Kanda Maalumu, ni ‘special’ (maalumu), kesi ziko chini ya
kanda hiyo,” alisema Mwasipu.
Alipoulizwa
kuhusu hali ya mbunge huyo ambaye awali aligoma kula na suala la
dhamana, Mwasipu alisema hivi sasa anakula na alihojiwa kwa takribani
saa moja, lakini dhamana yake ilishindikana.
“Suala
la kufikiswa mahakamani ama kutofikishwa mahakamani hilo ni suala lao
polisi, lakini maelezo kaandika na tulifuatilia suala zima la dhamana
ikawa ngumu.
“Walisema
wao hawana maelekezo yoyote kuhusu dhamana, ni wale ambao walikuwa
wanamsimamia Halima kuandika maelezo, hadi jioni hii walinipigia simu,
kimsingi leo hatapata dhamana, labda kesho,” alisema Mwasipu.
Awali,
waandishi wa MTANZANIA Jumapili walifika kituoni hapo, lakini walizuiwa
getini baada ya kujitambulisha kwa madai kuwa Kaimu Kamanda wa Kanda
Maalumu hakuwapo ofisini na wala hakukuwa na mtu mwingine aliyekuwapo
ili kutoa taarifa kwa waaandishi wa habari na kutakiwa kusubiri nje ya
eneo la kituo.
Wakiwa
nje ya kituo hicho ambako walikaa kwa saa kadhaa, walishuhudia hali ya
utulivu huku ukaguzi ukiendelea, huku baadhi ya watu waliosadikika kuwa
wafuasi wa Chadema walizuiwa kuingia na kukaa kando kwa muda kabla ya
kuondoka.
Mdee,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha),
alikamatwa Julai 4, mwaka huu, baada ya Hapi kutoa amri ya kushikiliwa
kwa saa 48 kutokana na matamshi aliyodai kuwa ni ya kumkashifu Rais Dk.
John Magufuli.
Matamshi hayo anadaiwa kuyatoa katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni, Dar es Salaam.
Mdee
alidaiwa kumkashifu Rais Magufuli kutokana na kuhoji baadhi ya kauli
zake zikiwamo zile alizotumia wakati akitangaza kupiga marufuku
wanafunzi wa kike wanaopata mimba kurejea shuleni.
Si hilo tu, Mdee pia alihoji kauli nyingine zinazotolewa na Rais Magufuli ambazo alidai kuwa zinakiuka misingi ya sheria.
No comments:
Post a Comment