Stars yapania kuisambaratisha Lesotho
Timu ya taifa ya mpira wa
miguu ya Tanzania, Taifa stars imeanza kujifua kwa mazoezi mazito usiku
wa jana mara tu baada ya kufika salama mjini Alexandria, nchini Misri
kwa ajili ya kuweka kambi ya wiki moja.
Kocha mkuu wa Taifa Stars Salum Mayanga aliyeshika kiuno akiwa na viongozi wa TFF wakikagua uwanja wa mazoezi hapo jana nchini Misri.
Kocha Mayanga ambaye alipewa majukumu ya kuifundisha timu hiyo mapema Januari, mwaka huu, amesema:
"Programu ya mazoezi kwa timu itakuwa zaidi usiku kwa sababu mchezo
wetu dhidi ya Lesotho pia utachezwa usiku, hii ni kutokana na mfungo wa
mwezi mtukufu wa Ramadhan ingawa wakati mwingine mazoezi yatafanyika
asubuhi na jioni."
Taifa Stars inayopiga kambi nchini Misri, inajiandaa na mchezo dhidi
ya Lesotho utakaofanyika Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Azam Complex
ulioko Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mchezo huo umepangwa
kuanza saa 2.00 usiku.Mchezo dhidi ya Lesotho ni muhimu kwa Tanzania ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi 'L' kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika nchini Cameroon.
Mbali ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi 'L' ni Uganda na Cape Verde ambao pia wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa katika mchezo wa kwanza pia kuwania nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment