Changamoto za Simba zitanikuzia kipaji
Beki wa Kulia wa Klabu ya Simba
aliyekuwa akiitumikia Klabu ya Azam FC Shomary Kapombe amewataka
mashabiki kuendelea kumpa sapoti katika msimu ujao wa Ligi kuu ya Soka
Tanzania Bara.
Kapombe
amesema anaamini kutakuwa na ushindani mkubwa ndani ya Klabu ya Simba
ambayo alishaitumikia kabla ya kujiunga na Azam FC lakini anaamini
changamoto hizo zitamfanya kuwa mchezaji bora zaidi na kuweza kukuza
kipaji chake.
“Unajua kufanya maamuzi kama
nilivyofanya mimi inatakiwa kuwa na ujasiri, kwani sisi wachezaji
tunakuwa na wakati mgumu sana katika kufanya maamuzi kipindi hiki cha
usajili, nimetoka Azam FC na kulikuwa na changamoto kubwa ndani na nje
ya Klabu, kwa sasa narejea tena Simba na nilianza kuifuatilia tangia
msimu uliopita, nilikuwa naiona na naendelea kuiona kwani inawachezaji
na benchi la ufundi zuri na naona kunachangamoto kubwa pia ambayo
zitanifanya mimi kuendelea kuwa mchezaji mzuri, ” amesema.
“Naamini kiwango changu na
ndoto zangu zitaendelea kuwa juu kwani nakutana tena na wachezaji wazuri
kama nilipotoka na najua kutakuwa na ushindani mkubwa sana wa namba
kwahiyo nimejiandaa na nachukulia changamoto nitakazokutana nazo ndizo
zitanipa mafanikio zaidi, ” Kapombe aliongeza.
Shomary amewashukuru uongozi pamoja na
mashabiki wa Azam FC kwakuwa naye pamoja na kukiboresha kikosi chake kwa
muda wote aliokuwa nao.
“Naushukuru uongozi na
mashabiki wa Azam FC kwani najua mchango wao kwangu pia mengi mazuri
waliyonitendea, na hapa nilipofikia ni kwa ajili ya Azam FC kwani
wamekiwezesha kipaji changu kufikia hapa na naamini nitafika mbali
zaidi, ” amesema.
Shomary Kapombe aliitumikia Klabu ya
Azam FC kwa miaka mitatu akitokea AS Cannes ambayo alienda akitokea
Simba SC na sasa amerudi tena katika Klabu ya Simba kwa mkataba wa miaka
miwili.
No comments:
Post a Comment