Trending News>>

KUTOKA BUNGENI: RAMBIRAMBI ZA WATOTO WA LUCKY VICENT ZAZUA BALAA ZITO BUNGENI..


SAKATA la matumizi ya fedha ya rambirambi iliyochangwa kwa lengo la kuwafariji wafiwa wa wanafunzi 32 na wafanyakazi watatu wa Shule ya Lucky Vincent ya jijini Arusha, limetinga bungeni baada ya watunga sheria kutaka maelezo kwa nini fedha hiyo imeelekezwa kwenye matumizi ya serikali.
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), ndiye aliyelifikisha suala hilo bungeni mjini hapa jana aliposimama na kuomba mwongozo wa Kiti cha Spika kuhusu matumizi ya fedha hizo mara tu baada ya kumalizika kwa kipindi cha ‘Maswali na Majibu’.
Katika kujenga hoja yake, mbunge huyo alisema amepata taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba, fedha ya rambirambi imeelekezwa katika ukarabati wa Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo wako kwa kutumia Kanuni ya 68(7) kinachohusu jambo lilijitokeza mapema bungeni. Nilikuwa hapo nje, nimeangalia magazeti yanaelezea matumizi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya rambirambi na kuwafariji wafiwa wa watu waliofariki katika ajali ya basi la Shule ya Lucky Vincent zimetumika kinyume cha malengo yake,” alisema.
“Madaktari wamelipwa kama posho na fedha zingine zinakarabati Hospitali ya Mount Meru, tofauti na ilivyokusudiwa. Katika hili, Bunge linahusika kwa maana tulikatwa posho hapa ili kusaidia familia za wafiwa, ilikuwa misaada kwa wahusika. Sasa hii tabia imekuwa ikijirudia.”
Alisema wananchi wamekuwa wakichanga kwa lengo la kusaidia waathirika lakini serikali imekuwa haifikishi fedha hizo kwa walengwa.
“Tabia hii imekuwa ikijirudia mara kwa mara, jambo ambalo si zuri kwani watu wataacha kuchanga wakijua kwamba fedha hazisaidii walengwa,” alisema na kufafanua zaidi:
“Tabia hii inanikera hata mimi mwenyewe, kama tutakuwa tunachanga fedha za rambirambi halafu inabadilishwa matumizi juu kwa juu bila hata wahusika kupelekewa.

No comments:

Powered by Blogger.