Serikali kupangua sheria zinazokwamisha uwekezaji
Serikali imesema inazitambua changamoto zinazowakabili waajiri nchini ikiwemo uwepo wa tozo mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka tofauti za Serikali kwa huduma ileile, na kusema itazifanyia mapitio sheria zinazoweka changamoto hizo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa tayari mchakato wa kuainisha sheria zote zinazoonekana kukwamisha uwekezaji pamoja na mazingira ya biashara nchini umeanza.
Ametoa kauli hiyo jana usiku kwenye sherehe za utoaji wa tuzo ya muajiri bora wa mwaka 2016, zilizofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Tuzo hizo zimeandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE).
“Lengo letu ni kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini ili yaweze kuvutia zaidi na mchakato huu unashughulikiwa na Wizara ya Fedha na Mipango. Tunaomba mvumilie na mshirikiane nasi katika kuendelea kuziainisha sheria zinazokwaza biashara ili tuweze kuzijumuisha kwenye mapitio hayo,” alisema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwashauri waajiri wote nchini waendelee kufanyakazi zao kwa mujibu wa sheria ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima mahala pa kazi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk. Aggrey Mlimuka alisema lengo la uaandaji wa tuzo hiyo ni kutambua wanachama wenye sera nzuri za usimamizi wa rasilimali watu katika taasisi na makampuni mbalimbali mwanachama hapa nchini.
Dk. Mlimuka alisema kuwa tuzo hio pia ilijikita zaidi katika kuangalia maeneo muhimu ya rasilimali watu, uongozi, utawala, usimamizi wa Rasilimali watu, kusaidia jamii pamoja na kuwajibika katika jamii, ubora na uzalishaji.
No comments:
Post a Comment