Maswali 7 Tata Kumhusu Scorpion
Mtuhumiwa Salum Henjewele ‘Scorpion’.
NDUGU NA MARAFIKI WANALIJUA JINA LA SCORPION?
Jina la Scorpion lilianza kuvuma tangu siku ya tukio, watu mbalimbali
wakimtaja kwamba ndiye mtuhumiwa wa ukatili huo na kwamba alikuwa
maarufu mitaa yote ya Buguruni lilikotokea tukio hilo.
KWA NINI ALICHAGUA JINA LA SCORPION?
“Alilichagua jina hilo kwa sababu watu wengi wa karate wanapenda kujiita
majina kama hayo. Mfano mimi mwalimu wake najiita Dragon. Kuna mwingine
ambaye ni baunsa wa kiongozi mmoja wa chama cha siasa nchini…(anamtaja
jina) yeye anajiita Cobra. Kifupi ni kwamba, wacheza karate wengi
duniani wana majina nje ya kwao ya asili na wengi hupenda kutumia majina
ya wanyama au wadudu,” alisema mwalimu wa karate wa Scorpion al iyej i
tambul i sha kwa jina la Kaizile Jabiry.
ANA A.K.A NYINGINE?
Kuhusu hilo, muandaaji wa sinema za Bongo, Tuesday Kihangala ‘Mr. Chuz’ alisema:
“Mbali na Scorpion, mimi nalijua jina la Samjet. Hili jina alilitumia
zaidi kwenye mazoezi yake ya karate kwani alipenda kuruka juu kama ndege
f’lani hivi. Si unajua tena.”
NI KWELI ALIKUWA BAUNSA WA KIMBOKA?
Kimboka ni baa maarufu iliyopo eneo la Buguruni- Sheli. Muda mfupi baada
ya kutokea kwa tukio hilo, yalisambaa madai mitaani kwamba, Scorpion
alikuwa mlinzi (baunsa) katika baa hiyo na alikuwa akitumainiwa kwa
kuwadhibiti vibaka na wahalifu katika eneo hilo.
Hata hivyo, akiongea na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita, mfanyakazi
mmoja wa baa hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Manka, alisema
hamjui Scorpion.
NI MKAZI WA WAPI?
Muda mfupi baada ya tukio la Scorpion kudaiwa kumjeruhi Said na kumtoboa
macho, watu mbalimbali waliohojiwa, walidai kwamba, mtuhumiwa huyo ni
mkazi wa Buguruni- Kwamnyamani na kwamba ni maarufu maeneo hayo na kuwa,
hakuna mtu ambaye hamjui.
“Kiukweli hata hafahamiki makazi yake halisi ni wapi ila hakai Buguruni,
Yombo wala Tabata, hata watu wake wa karibu ukiwauliza, hakuna anayejua
anaishi wapi,” kilisema chanzo chetu, maelezo ambayo yalipewa nguvu na
mwalimu wake, Kaizile ambaye alisema licha ya kuwa naye karibu kwa
kipindi kirefu, hakujua anakoishi.
Baadaye, baadhi ya vyombo vya habari vikaripoti kwamba Scorpion ni mkazi wa Yombo na vingine vikisema ni mkazi wa Tabata.
Lakini kwa mujibu wa taarifa za kimahakama, mtuhumiwa huyo ni mkazi wa
Buguruni- Machimbo jijini Dar es Salaam hivyo umaarufu wake maeneo ya
Buguruni uko wazi.
JE, NI TUKIO LA KISASI?
Katika tukio hilo, baadhi ya watu waliozungumza na Uwazi walidai ukatili
aliofanyiwa Said si wa kawaida na kwamba, kuna kitu kinafichika nyuma
ya pazia huku wengine wakidai kuna dalili za kisasi.
Pia ACP Salum alilifafanua hilo: “Kwa kweli mimi sijaweza kuthibitisha
motive (sababu au kisa) hasa kuwa ni nini. Lakini mimi naona ni uhalifu
wa kawaida tu.”
AMEOA, HAJAOA?
Miongoni mwa maswali tata kuhusu mtuhumiwa huyo, lilikuwa ni kama ameoa
au anaishi mwenyewe ambapo kila mtu alikuwa akizungumza lake. Lakini
baada ya uchunguzi wa Uwazi, imebainika kwamba, Scorpion amewahi kuoa
lakini baadaye akaachana na mkewe. Kwa hiyo mpaka tukio hilo linatokea,
alikuwa akiishi mwenyewe.
Maelezo hayo yalipewa nguvu na Mr Chuz aliyethibitisha kwamba Scorpion amewahi kuoa lakini ‘akazinguana’ na mkewe, wakaachana
WACHUNGAJI WAMUITA MAJERUHI MAKANISANI
Wakati huohuo, kuna habari kwamba, baadhi ya wachungaji wa makanisa ya
kiroho nchini, wamemuita kijana aliyetobolewa macho, Said kuhudhuria
ibada kwenye makanisa ili kumwombea apone na kuweza kuona tena licha ya
madaktari wa Hospitali ya Taifa, Muhimbili kusema hawezi kuona tena!
“Unajua kidaktari ni sawa kabisa, hawezi kuona tena maana ameondolewa
hadi goroli. Lakini kwa Mungu goroli zinaweza kurudi kwani yeye si ndiyo
muumbaji bwana! Nini kwake kinashindikana?” alisema mchungaji mmoja wa
kanisa la kiroho lililopo Temeke aliyejitambulisha kwa jina moja la
Mathayo.
MAMA RWAKATARE: ANAWEZA KUONA TENA ENDAPO…
Naye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Mlima wa Moto Assemblies of God,
Mikocheni B, mama Getrude Rwakatare alipoulizwa kuhusu wachungaji
kumuita majeruhi huyo ili kumwombea, alisema:
“Mimi siyo Mungu na wala si mponyaji. Kama anakuja kanisani nikatoa neno
mimi au akaenda makanisa mengine kwa imani yake kwamba Mungu anaweza
kumponya, anaweza kuona tena! Lakini iwe kwa imani yake na si kwa
kujaribu.
Kauli ya mama Rwakatare inaongezewa nguvu zaidi na mchungaji mwingine wa Kanisa la Bwana lenye makao yake, Ilala, Dar, Ezekiel Mhaga ambaye alisema kuwa Said kuona tena si suala la kutilia shaka endapo mwenyewe atakuwa na imani.
“Kwani Said ni nani hata Mungu asimtendee muujiza wake wa kuona tena? Tena basi, Mungu anapenda kujiinua pale ambapo, uwezo wa binadamu na utaalam wa elimu umeshindwa,” alisema mchungaji huyo.
YAMEKUJAJE HAYA?
Kauli za watumishi hao wa Mungu, zimekuja kufuatia majibu ya madaktari wa Hospitali ya Muhimbili ambapo Said alipelekwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kusema uchunguzi wao umebaini kuwa majeruhi huyo hawezi kuona tena, hali iliyoibua vilio kwa mhusika na mkewe.
Imeandikwa na Hashim Aziz, Gabriel Ng’osha, Leonard Msigwa na Sifael Paul.
No comments:
Post a Comment