Trending News>>

Teknolojia Kombe la Dunia yaibua Mjadala

Chumba cha matumizi ya kiteknolojia katika uamuzi wa soka 'video assistant refereeing' (VAR) katika kituo rasmi cha kupeperusha michuano ya Kombe la Dunia Urusi 2018 jijini Moscow Juni 9, 2018. Picha/AFP 

Fainali za Kombe la Dunia zinaendelea Urusi na zitafikia tamati Julai 15.


DAR/MASHIRIKA


MATUMIZI ya teknolojia ya mashine ‘VAR’, yameanza kuibua mjadala kila pembe za dunia baada ya kuonekana sio suluhisho la kuamua utata wa mabao au adhabu katika mchezo wa soka.

‘Video Assistant Referee’ (VAR), imeanza kutumika kwa mara ya kwanza katika Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Urusi.

Mbali na makocha, wachezaji, utata wa matumizi ya VAR, umewaibua wachambuzi na nyota wa zamani waliowahi kutamba katika soka duniani.

Pia watu mbalimbali wakiwamo wadau wa michezo nchini, wameonyesha wasiwasi wao kuhusu matumizi ya teknolojia hiyo.

Wachambuzi mahiri katika televisheni Uingereza, Ian Wright, Roy Keane, Mark Clattenburg, na Gary Neville wameeleza kukerwa na matumizi ya teknolojia hiyo walipokuwa wakichambua mchezo kati ya Uswisi na Brazil.

Walisema kama sio matumizi ya tekonolojia hiyo, Brazil ingeibuka na ushindi kwa kuwa VAR ndiyo iliyoisaidia Uswisi kupata bao la kusawazisha na mechi hiyo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Bao la Uswisi lililofungwa na Steven Zuber lilikubaliwa baada ya kusubiri VAR kuamua kama ni bao halali au vinginevyo.

“Katika hali ya kawaida kama sio matumizi ya VAR bao la kusawazisha la Uswisi lisingekubaliwa kwa kutumia waamuzi wasaidizi kwa sababu wao wanasita kutoa uamuzi katika mazingira ya sasa kuhofia kwenda kinyume na VAR,” alisema Wright; nyota wa zamani wa Arsenal.

Mchambuzi huyo alifafanua kuwa mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Rostov Arena haukuwa na ‘ladha’ kutokana na matumizi ya VAR kwa kuwa muda mrefu waamuzi wasaidizi walisubiri uamuzi kutoka VAR hata pale wachezaji wa Uswisi walipocheza rafu dhidi ya mastaa wa Brazil.

Naye Clattenburg alisema ni vyema VAR ikaondolewa katika matumizi kwa sababu inaonekana inaondoa ‘ladha’ ya soka mbali na kuinyima ushindi timu iliyostahili kama ilivyotokea kwa Brazil.

Wachezaji wa Brazil walipinga bao la Zuber wakimlaumu mwamuzi Cesar Ramos kufumbia macho kitendo cha mfungaji kumsukuma beki wao Miranda kabla ya kupiga kichwa mpira uliojaa wavuni.

Utata wa VAR ulionekana pia katika mchezo kati ya Ufaransa na Australia, uliopigwa Uwanja wa Kazan Arena, ambapo mwamuzi Andres Cunha, alipeta na mpira uliendelea kwa takriban dakika mbili kabla ya kuelezwa na wasaidizi wake kuhusiana na kile kinachoonekana katika marudio ya tukio na kubadili uamuzi.

Mwamuzi huyo alipiga filimbi ya kusimamisha mchezo na kuamuru ipigwe penalti kwa upande wa Ufaransa na Antoine Griezmann alifunga bao la kuongoza kabla ya Mile Jedinak kusawazisha sawa na mchezo wa Jumatatu ambapo Uswidi ilipata penalti kama hiyo dhidi ya Korea Kusini.

Mjadala wa matumizi ya teknolojia hiyo umewaibua waamuzi waandamizi wa zamani nchini akiwamo Leslie Liunda.

Liunda ambaye ni mkufunzi wa waamuzi anayetambuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), alisema kwa upande mmoja matumizi ya teknolojia hiyo yana faida na wakati mwingine ni hasara.

“Kwangu mimi kama mwanafamilia wa mpira wa miguu, naamini suala la matumizi ya teknolojia ni njema na la kimaendeleo kwa sababu linasaidia katika kumpunguzia majukumu mwamuzi ingawa tukumbuke kuwa bado yenyewe haitoi uamuzi isipokuwa wanaoamua ni marefa.

Inawezekana kila mtu akawa na maoni yake lakini ya mwamuzi ndio ya mwisho, inawezekana mashabiki kwa maoni yao wakahisi Brazil kwa mfano ilistahili kupata penalti lakini mwamuzi wa kati kulingana na sehemu aliyokuwepo na kwa maoni yake akaona sio penalti.

“Hata hivyo, tunapaswa kukumbuka hii ni teknolojia mpya na changamoto kama hizi Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) linaziona na litazifanyia kazi ingawa kwa mtazamo wangu, utata unapotokea kama hivi ndio uhondo hasa wa mchezo wa soka,” alisema Liunda.

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Chama alisema ingawa matumizi ya teknolojia ya video yana umuhimu wake, bado hayawezi kumaliza utata kwenye mchezo wa soka.

“Kama ambavyo kila siku nasema mwamuzi wa mchezo wa mpira wa miguu sio sawa na hakimu au Jaji wa mahakama. Refa anatakiwa atoe uamuzi wake kwa haraka zaidi tofauti na inavyokuwa mahakamani ambako Jaji au Hakimu anaweza kujipa muda wa kujiridhisha zaidi.

Zaidi ya yote, katika matumizi ya teknolojia, waamuzi wanabaki kuwa binadamu wanatofautiana namna ya kulielewa na kulitafsiri tukio,” alisema Chama.

Katibu Mkuu wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT), Oden Mbaga alisema haamini kama matumizi ya teknolojia yatasaidia kutatua matukio ya utata.

“Matumizi ya video katika kuwasaidia marefa, yanafanya wazidi kupoteza umakini kwa kujiamini kuwa watasaidiwa na teknolojia hiyo tofauti na zamani,” alisema.

No comments:

Powered by Blogger.