POINTI TATU ZA YANGA ZAYEYUKA ANGANI.
Kamati ya Bodi ya Ligi Kuu Bara imegoma kuipa klabu ya Yanga pointi tatu ambazo mashabiki wengi wa klabu hiyo walitegemea kuzipata kufuatia makosa kadhaa yaliyofanywa na klabu ya Mbeya City katika mchezo wa ligi kuu namba 199 uliochezwa katika dimba la Sokoine jijini Mbeya.
Katika mchezo huo matukio mbalimbali yaliripotiwa ikiwa ni pamoja na mashabiki wa Mbeya City kurusha mawe uwanjani, kitendo kilichopelekea mchezo huo kusimama kwa takribani dakika 5, na kisha kuendelea mara baada ya hali kutulia uwanjani hapo.
Tukio lingine ni lile la mchezaji wa Mbeya City aitwaye Ramadhani Malima kurudi uwanjani kushangilia goli la kusawazisha kwa upande wa Mbeya City lilofungwa na mchezaji Iddi Nado, ilihali mchezaji huyo akiwa na kadi nyekundu aliyozawadiwa na kwenda nje ya mchezo.
Baada ya matukio hayo yote, uongozi wa klabu ya Yanga uliamua kuandika barua kwenda bodi ya ligi ikilalamikia kutokea kwa matukio hayo, ambapo walidai wanastahili kupewa pointi tatu mara baada ya timu ya Mbeya City kukiuka sheria na kanuni za soka katika mchezo wao huo.
Ikitangaza majibu ya barua hiyo ya Yanga, Bodi ya Ligi imesema matokeo ya mchezo huo yanabaki kama yalivyo, yaani sare ya 1-1, na hivyo Yanga kusalia na pointi yake moja iliyovuna katika mchezo huo.
Hata hivyo mchezaji Ramadhani Malima amesimamishwa kucheza michezo yote iliyosalia mpaka suala lake litakapojadiliwa na kamati hiyo.
No comments:
Post a Comment