NI MADRID TENA FAINALI UEFA CHAMPIONS LEAGUE
Klabu ya Real Madrid ya nchini Hispania imefanikiwa kutinga katika hatua ya fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya (UEFA) mara baada ya kuindoa timu ya Bayern Munich ya Ujerumani kwa jumla ya magoli 4-3.
Katika mchezo wake uliochezwa usiku wa kuamkia leo, Madrid imetoka sare ya kufungana bao 2-2 na Bayern, matokeo yaliyoifanya timu hiyo kutinga hatua ya fainali kufuatia faida ya magoli 2-1 iliyoyapata kwenye mechi ya ugenini nchini Ujerumani.
Hii inakuwa mara ya tatu mfululizo kwa Real Madrid kutinga hatua hii ya fainali, kwani hata miaka miwili iliyopita timu hii imekuwa ikipata bahati ya kutinga katika hatua hii, na safari hii itakutana na kati ya timu ya Liverpool ama Roma katika mchezo wa fainali utakaopigwa Mei 26 mwaka huu mjini Kiev katika nchi ya Ukraine.
Hata hivyo Bayern watapaswa wajilaumu kupoteza mchezo huu kwani wao ndio walikuwa wa kwanza kupachika goli katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Joshua Kimmich kabla ya Karim Benzema kuisawazishia Madrid baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Marcelo.
Makosa ya mlinda mlango wa Bayern Sven Ulreich yaliizawadia Madrid goli la pili lililopachikwa na Benzema kabla ya James Rodriguez kusawazisha, na hadi mwisho wa mchezo Madrid 2 na Bayern 2.
No comments:
Post a Comment