Trending News>>

HUU NDO UKWELI SAKATA LA MOND VS WAZIRI


Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’
HALI imechafuka na mambo si shwari hata kidogo! Sakata la majibizano kati ya mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’ na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, limezidi kuchukua sura mpya, Ijumaa linakuletea ukweli kamili wa mtiririko wa majibizano hayo.
Mvutano huo ulianza kutimua vumbi mapema wiki hii na kukamata vilivyo kwenye mitandao ya kijamii huku kukiwa na mpasuko mkubwa wa kimtazamo kutoka kwa watu wa kada mbalimbali.

WAZIRI ALIKURUPUKA?
Akihojiwa katika Kipindi cha The Playlist cha Kituo cha Redio Times FM cha jijini Dar, Diamond alimtuhumu Waziri Shonza kufungia nyimbo za wasanii zikiwemo zake mbili za Halelluyah (aliowashirikisha Morgan Heritage) na Wakawaka (aliomshirikisha Rick Ross) bila kuzingatia hasara na usumbufu wanaoupata wakati wa kuziandaa kwa madai kuwa alikurupuka tu kutoka nyumbani kwake na kuchukua hatua hiyo.

HAWA HAWAJAFURUKUTA
Wengine waliofungiwa nyimbo zao zilizo kwenye mabano ni Nay wa Mitego (Pale Kati Patamu na Maku Makuz), Roma Mkatoliki (Kibamia), Man Fongo (Hainaga Ushemeji), Nikki Mbishi (I am Sorry JK), Snura Mushi (Chura na Nimevurugwa), Madee (Tema Mate Tuwachape), Jux (Uzuri Wako), Gigy Money (Papa) na Barnaba (Nampaga) ambao wao hawakufurukuta mbele ya serikali.
Baada ya mahojiano hayo, Ijumaa lilizungumza na watu mbalimbali ili kupata mitazamo yao kama Diamond alikuwa sahihi au la juu ya sakata hilo.

JOYCE CHARLES WA KARIAKOO: “Diamond kumtishia waziri ni kiburi cha fedha, unajua sasa hivi ana fedha hivyo anaona ameshayapatia maisha bila kujua serikali ina mkono mrefu.”
YONA PLATNUMZ WA MBAGALA: “Kinachoonekana huyo waziri anaonea
wasanii maana hata wale wengine waliofungiwa wamekuwa wakilalamika sema tu wao hawajapewa kipindi kwenye redio kama alivyopewa Diamond pale Times FM.”

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza,



PAMELA DIVA WA SINZA:
“Kwa vyovyote kuna kitu nyuma ya pazia maana Diamond hajawahi kuwa mwepesi kiasi hicho cha kurusha povu kwa viongozi wa serikali, sisi yetu macho, lakini naamini kabisa kuna kitu kikubwa au kuna mkubwa anampa kiburi Diamond.”

SIWEMA WA MAKUMBUSHO:
“Diamond hana lolote, ni mzee wa  fursa, ameona kiki ya Zari kuuzia album imegoma sasa kaibuka na Waziri Shonza.”
RAYVANNY WA WCB:
“Mara nyingi thamani ya mtu na umuhimu wa mtu wengi wanaujua akishaondoka… muziki ni kazi na ni ajira, ninamaanisha kuna familia nyingi zinaishi kupitia muziki huuhuu.
“Katika wasanii wote Diamond amekuwa chachu ya kuongeza thamani ya muziki, kumbuka…ili mbegu iote, lazima ioze.”

QEEN DARLEEN WA WCB:
“Wakati baadhi ya watu nchini kwetu wanapambana kukushusha, nchi ya jirani inatamani kuwa na msanii kama wewe.”
FAIZA ALLY:
“Mungu akutunze baba.”

AUNT EZEKIEL:
“Woga wako ndiyo kufeli kwako Diamond…I’m so proud of you kiukweli unajua unachokifanya, haijalishi anayetaka kukukatisha safari yako ni nani na ana cheo gani! Ilimradi unajua haki yako, basi huweka woga pembeni na kutetea haki yako…safi sana…”
WAZIRI SHONZA SASA
Kufuatia kuwepo kwa maoni hayo lukuki kwenye mitandao ya kijamii, ‘hotuba’ hiyo ya Diamond ilikuwa haivumiliki kwani pamoja na kusema kuwa hataki kujibizana na msanii huyo, Waziri Shonza alimjibu:
“Siwezi kumjibu kwa sababu zipo taratibu za kufuata kama msanii hajatendewa haki.”
Katika maelezo yake, Waziri Shonza alisema kama kuna msanii anayeona hakutendewa haki, milango iko wazi kuandika barua ya malalamiko.
Alisema kuwa, wasanii wanapaswa kuelewa kwamba hakuna aliye juu ya sheria hata kama ni msanii mkubwa kiasi gani.

DIAMOND TENA
Baada ya kusema hayo, Waziri Shonza alizua mjadala mpya kwani Diamond alimjibu tena kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa hata yeye (naibu waziri) alipaswa kuwaandikia barua wasanii kuhusu kuwafungia nyimbo zao.

MWAKYEMBE AMSHAMBULIA
Pamoja na Diamond kummwagia sifa kemkemu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuwa amekuwa msaada mkubwa kwa wasanii kwa kuwashauri badala ya kuwafungia nyimbo zao, lakini naye alimshambulia msanii huyo kwa kitendo chake cha kumdhalilisha Waziri Shonza kwenye vyombo vya habari.
Juzi, Waziri Mwakyembe alionesha kukerwa na Diamond kutokana na kumshambulia naibu wake na katika maelezo yake, Mwakyembe alisema inaelekea sasa Diamond ameanza kusumbuliwa na umaarufu.
Kuhusu hoja ya vikao alivyodai mwanamuziki huyo kuwa huwa anakaa nao, Mwakyembe alisema:
“Kama ni vikao na wasanii, tumefanya vingi sana, lakini Diamond hahudhurii vikao hivyo na si wajibu wa serikali kumfanyia kikao chake mwenyewe, haijalishi ni maarufu kiasi gani.
“Hatuwezi kuwa na sheria kwa wasanii wengine na sheria maalum kwake, nadhani hizi ni dalili za kuanza kulewa umaarufu kwani Diamond si Kiongozi wa Shirikisho la Muziki wala msemaji wa Chama cha Muziki wa Kizazi Kipya kuwasemea wenzake.”

USHAURI WA MWAKYEMBE
Waziri Mwakyembe alimshauri Diamond: “Si busara kwake kushindana na serikali na kama ana ushauri, basi autoe kistaarabu utazingatiwa, lakini si kwa kumshambulia naibu waziri kwa dharau na kejeli jinsi alivyofanya. Sijafurahishwa hata kidogo.”

BASATA NAO
Kwa upande wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kupitia kwa katibu wake mkuu, Godfrey Mngereza lilisema kuwa, Diamond amefanya makosa kumjibu Waziri Shonza kwani huko ni sawa na kuitukana serikali.
“Maneno machafu anayoyatoa dhidi ya naibu waziri ni sawa na kuitusi serikali, jambo ambalo hata ukienda katika sheria za kimtandao, anaweza kujikuta anaingia matatizoni,” alisema Mngereza.

ALIANZIA KENYA
Kabla ya mambo hayo yote, Diamond alianza kumlalamikia Waziri Shonza wiki iliyopita akiwa nchini Kenya kwenye uzinduzi wa albamu yake ya A Boy From Tandale ambapo alikuwa akihojiwa na Kituo cha Redio cha Classic FM cha nchini humo.
Alidai kuwa, viongozi hawafanyi utafiti kabla ya kutoa uamuzi.
“Naibu waziri amenizidi elimu, umri, mamlaka na vitu vingi, lakini kwenye elimu ya sanaa nimemzidi hivyo alipaswa kunisikiliza kabla ya kufungia nyimbo zangu.”

NINI KIFANYIKE?
Ni vizuri jambo hili likahitimishwa kwa kuwaweka chini wahusika wote na kuwapa kanuni na taratibu za kiutendaji na sheria ya kuzifungia nyimbo ili naibu waziri aachane na malumbano haya kwani Watanzania hawayahitaji na badala yake wanataka maendeleo.

No comments:

Powered by Blogger.