SIMBA SC: NYUMA ZEGE MBELE KIWEMBE
SIMBA imewafanya mashabiki wake kuanza kunenepa na kutembea kifua mbele mitaani kutokana na raha inayowapa kwenye Ligi Kuu Bara.
Kasi ya timu hiyo inayoongoza msimamo kwa pointi 32 baada ya mechi 14, imewafanya mpaka mabosi wake kupagawa na kiwango cha timu hasa kutokana na kuwa moto mbele na huku ukuta wao ukiwa kama uliosakafiwa kwa zege.
Ipo hivi. Simba chini ya Kocha Msaidizi, Masudi Djuma aliyekuwa akikaimu nafasi ya Kocha Mkuu baada ya Joseph Omog kutupiwa virago, imetumia dakika 270 bila kuruhusu wavu wao kuguswa huku ikigawa dozi nene kwa wapinzani na kuwasisimua Wana Msimbazi.
Katika mechi tatu mfululizo Simba imeziumiza Ndanda, Singida United na Kagera Sugar, tena mechi mbili zikiwa za ugenini na moja tu ya nyumbani kitu ambacho hakikuwa cha kawaida.
Wakati mabosi wa Simba wakianza kuwaza uwezekano wa timu yao kumaliza ukame wa mataji ya Ligi Kuu walilolikosa kwa miaka mitano mfululizo, lakini ugumu wa safu ya ulinzi imefanya iwe gumzo kubwa.
Tangu Djuma alipoanza kutumia mfumo huo kwenye mechi dhidi ya Ndanda, Simba sasa imecheza dakika 270 bila kuruhusu bao huku ikifunga mabao manane katika michezo hiyo.
Ushidi huo ni ule wa 2-0 dhidi ya Ndanda na Kagera Sugar pamoja na kipigo cha maana cha mabao 4-0 ilichotoa kwa Singida United.
Djuma alisema anafurahi kuona mfumo huo umekubali hasa katika ulinzi na ushambuliaji jambo ambalo limewawezesha kupata matokeo makubwa.
“Mfumo umekwenda vizuri sasa, tulishindwa kufanya vizuri sana wakati wa Mapinduzi lakini sasa tunakwenda sawa, unaweza kuona katika mechi tatu tumepata mabao manane na hatujafungwa hata moja,” alisema.
“Tumewapa uhuru baadhi ya wachezaji kama Nicholas Gyan na baadaye Shomari Kapombe, wanatakiwa kukaba, lakini wanaweza kwenda kushambulia muda wote, hii inaipa timu nguvu kubwa.
“Mfano Gyan ni mshambuliaji mzuri, lakini akicheza mbele anakamiwa sana, nimeamua kumpa uhuru wa kucheza kuanzia nyuma, amekuwa hatari zaidi,” alisema kocha huyo wa zamani wa Rayon Sports ya Rwanda.
“Kurejea kwa Kapombe ni nguvu kubwa sana kwetu. Nilimwahidi kwamba akifanya mazoezi kwa wiki tatu na timu nitampa nafasi, na umeona amekuwa mtu wa tofauti, amekuja kwa kasi,” aliongeza kocha huyo aliyerejesha mamlaka ya ukocha mkuu wa Mfaransa Pierre Lachentre.
Kadhalika inaonyesha kuwa Majimaji haijawahi kuisumbua Simba jijini Dar es Salaam, kitu kinachotoa ishara kwamba huenda rekodi ya vipigo ikaendelea kuandikwa keshokutwa Jumapili.
CHANZO MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment