Trending News>>

Ndemla anaing’arisha Simba, kwa kufanya kilichowashinda Kazimoto, Mzamiru, katika 3-5-2


NIMEANDIKA mara kadhaa kuwa Said Ndemla ni kiungo bora mchezesha timu Tanzania na ameshathibitisha hilo mara nyingi kuwa yeye ‘mpiga pasi bora za kupenyeza za umbali mrefu’ nchini. Ameshacheza michezo kadhaa msimu huu, lakini uwezo aliouonyesha katika michezo miwili iliyopita tangu alipochukua nafasi ya mzoefu Mwinyi Kazimoto dakika za mwanzo vs Singida United umemfanya ‘awe katika kiwango’ chake cha kawaida.
Mwanzoni mwa msimu huu niliandika makala na kuelezea namna kiungo-mchezesha timu Mzamiru Yassin anavyopaswa ‘kustuka’ kuhusu uchezaji wake ‘usiokua’ kwa manufaa ya timu yake. Ingawa walitokea watu waliopinga hoja yangu ile, sasa ‘hakika’ ushahidi wa mwisho kwa kiwango cha mchezaji huwa uwanjani.
Mzamiru alilazimika kuanzishwa benchi na kumpisha Ndemla katika mchezo muhimu ugenini vs Kagera Sugar siku ya Jumatatu hii, na kwa hakika Ndemla ameonyesha kuimarika katika kujiamini jambo ambalo amelikosa mara nyingi licha ya kuwepo klabuni hapo kwa mwaka wa sita sasa. Naamini kuna mengi mazuri yanakuja kutoka kwa Ndemla ‘Teko Modise wa Bongo’
Ndemla ni mchezaji ambaye kila anapopewa nafasi ya kucheza huwa tayari na hutoa mchango mkubwa kwa timu yake kwa sababu amekuwa akijiimarisha wakati wote katika viwanja vya mazoezi tofauti na wachezaji wengine. Kwa hakika nimekuwa nikifarijika kila napomuona kijana huyu akicheza kwani ni kati ya viungo ninaowahusudu sana ndiyo maana anapokuwa hapati nafasi ya kucheza Simba huwa namshauri aondoke kwani atang’ara sana sehemu nyingine-hasa Yanga.
Kutoa pasi mbili za magoli katika mchezo dhidi ya Singida United ambao alitokea benchi, kufunga goli muhimu la uongozi vs Kagera Suga FC katika uwanja wa Kaitaba, Bukoba ni sababu ya wengi kumzungumzia sasa na kuhoji kwanini alikuwa benchi, lakini huyu ni mchezaji anayetegemea kiwango cha timu nzima.
Kocha Masoud Djuma ambaye alikuwa akikaimu nafasi iliyoachwa na Joseph Omog ametumia mfumo wa 3-5-2 na kupata ushindi dhidi ya Ndanda FC 0-2 Simba, Simba 4-0 Singida, Kagera 0-2 Simba. Mfumo huu umemsaidia Ndemla kufanya kazi yake kwa urahisi-kuchukua mpira na kupiga pasi sahihi kwa washambuliaji akitokea kati ya uwanja.
Ni katika mfumo huu, Mwinyi Kazimoto alishindwa kufanya kazi aliyopaswa-kuchezesha timu na kupiga pasi za haraka akitokea kati mwa uwanja kuelekea katika mashambulizi. Wakati James Kotei na ‘nahodha asiyevaa beji’ Jonas Mkude wakitengeneza muunganiko mzuri-kuzuia na kuanzisha mashambulizi sahihi kutoka kwa safu ya ulinzi kuelekea mbele. Pasi zake timilifu zimeifanya Simba kucheza mchezo mzuri tofauti na wakati wa kocha Omog.
Mzamiru pia ameonekana kushindwa, yeye anashindwa kwa sababu pasi zake nyingi zinapotea huku pia akipiga katika mwelekeo usiostahili. Hapo ndipo nafasi ya Ndemla inapokuja na kama ataendelea kutumika hapo Simba itanufaika naye sana kwa maana Ndemla ni mchezaji asiyependa kupoteza muda wakati anapoona mwanya wa kupitisha pasi akiwa eneo lolote lile mchezoni.
Katika mchezo dhidi ya Kagera ambao alianzishwa sambamba na Mkude na Kotei, huku Gyan akitokea pembeni upande wa kulia na Asante Kwassi akitokea upande wa kushoto, Simba walikuwa salama sana na hata kama wasingefunga ilikuwa ngumu kwao kuruhusu goli.
Kuwa na mchezaji ‘sharp’ kimaamuzi katikati ya uwanja kama Ndemla ambaye tena anakabiwa na wenzake wanne ni faida kubwa mmno lakini ni lazima Mwinyi na Mzamiru nao wawe tayari na hili wanaweza kulifanya katika viwanja vya mazoezi ili kumsaidia kocha kupata wigo mpana wa kuchagua kikosi. Ndemla ni somo ‘lao’ usiku ndiyo darasa lao.

No comments:

Powered by Blogger.