Mwakyembe aagiza TFF ifuatilie uonevu ligi daraja la kwanza..
Taarifa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
inasema kwamba, Waziri mwenye dhamana ya Michezo Dk. Harrison
Mwakyembeameshtushwa na kusikitishwa na malalamiko ya wadau wa soka
nchini kuhusu vitendo vya uonevu na upendeleo vinavyodaiwa kujitokeza
kwa nguvu katika uendeshaji wa michezo ya ligi daraja la kwanzaTanzania
bara na ukimya wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) katika kufanyia kazi
malalamiko hayo ili kujenga afya njema ya mchezo wa soka Tanzania.
Katika salamu zake za mwaka mpya kwa Rais, Makamu wa Rais na Kaimu
Katibu Mkuu wa TFF, Dk. Mwakyembe amewataka viongozi hao kuchukua hatua
haraka kuchunguza kilichojiri katika mechi mbili zilizochezwa Jumamosi
tarehe 30 Disemba, 2017 kati ya Dodoma FC na Alliance ya Mwanza na kati
ya Pamba ya Mwanza na Biashara ya Musoma na kutoa maamuzi ya haki bila
kuangalia sura ya mtu ndani ya wiki hii bila kukosa.
“Watanzania wanahaki ya kujua kwa uwazi na ukweli msingi wa kadi nne
nyekundu kutolewa kwa wachezaji wa timu moja katika mchezo mmoja,
wanataka kujua kama kweli muda halali ulifuatwa kumaliza mchezo kati ya
Dodoma na Alliance , wanataka kujua kama kweli waandishi wa habari za
michezo walizuiwa kufanya kazi yao ya kikatiba ya kuwataarifu watanzania
wenzao kuhusu mmichezo hiyo miwili na kama ni kweli, nani aliwazuia,
wanataka kujua kama vitendea kazi vyao viliharibiwa na wahusika walikuwa
nani, wanataka kujua kauli za makamisaa wa mechi hizo mbili, wanataka
kujua faida ya kuendelea kuwa na Kamati ya Masaa 72 , na wanataka kujua
hisia za ujumla za watazamaji siku hiyo kuhusu usimamizi wa michezo hiyo
miwili”,Dk. Mwakyembe amesisitiza katika salamu zake hizo za mwaka
mpya.
Waziri Mwakyembe amesema pamoja na kwamba dhamana ya kusimamia na
kuendeshampira wa migu imekasimiwa kwa TFF, kama Waziri wa Sekta hiyo
hawezi kukaa kimya wakati tuhuma nzito za upendeleo na milungula
zinapoibuliwa, wakati TFF haishtuki mara moja na kuchukua hatua za
haraka.
“Tukiwa na mfumo mbovu uliosheheni mizengwe katika kupata timu bora
za kupanda daraja kuingia ligi kuu, tusahau kuwa ligi kuu yenye msisimko
na ushindani mkal”, amesema Waziri Mwakyembe.
Amewakumbusha viongozi wa TFF kuwa watanzania wameupokea uongozi wao
kwa imani, shauku na matarajio makubwa, hivyo wasiwavunje moyo kwa
kigugumizi cha kujitakia katika maamuzi. Wahakikishe kuwa kila tuhuma
inapatiwa maelezo ya kina na dhati, wakianza na tuhuma za upendeleo na
uonevu katika mechi mbili alizozitaja.
Amewataka viongozi hao wasipuuze chochote na kudhani watanzania
hawajui, la hasha wanajua ila wanawasogezea kamba polepole viongozi hao
wajinyonge wenyewe. Mathalani amesema, katika malalamiko waliyomletea
toka Jumamosi iliyopita kuhusu mechi hizo mbili, wananchi wanadai uwepo
wa kampeni ya makusudi upande wa viongozi wa TFF ya kuifanya timu ya
Dodoma iingie ligi kuu kwa udi na uvumba.
“Si dhambi kuiombea timu ya makao makuu ya nchi kuingia ligi kuu,
lakini si sahihi hata kidogo kwa viongozi kuibeba timu hiyo kama madai
hayo ni sahihi”, amesisitiza.
Aidha, tuhuma zingine ambazo hazina uthibitisho zinauhusisha uongozi
wa TFF kuzibeba timu za Coastal Union na timu ya Biashara ya Musoma.
No comments:
Post a Comment