Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kurudisha fedha ilizokata kimakosa kwa Mwalimu
Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema itarejesha kiasi
cha shilingi 282,000 ilizomkata kimakosa Mwalimu Edwini Ndyamukama wa
jijini Mwanza baada ya kugundua Mwalimu huyo hadaiwi na Bodi hiyo.
Taaarifa
iliyotolwa na Bodi ya Mikopo inaeleza kuwa kanzidata ya Bodi ya Mikopo
haimuoneshi Mwalimu Edwini Ndyamukama kama mdaiwa na baada ya uchunguzi
imebainika kuwa anayedaiwa na Bodi hiyo ni Edwin F. Ndyamukama aliyesoma
Chuo Kikuu Kishiriki cha Archbishop James (AJUCO) ambaye alikopeshwa na
kupokea zaidi ya Shilingi milioni 2.29 hadi kufikia mwaka 2015.
“Ni
kweli Mwalimu Ndyamukama mwenye namba ya mtihani wa Kidato cha nne
S0304.1993 anadai kurejeshewa shilingi 282,000 alizokatwa kama marejesho
ya mkopo wa elimu ya juu. Malipo haya na mengine yanakamilishwa na
yatawekwa katika akaunti yake ya benki kabla ya Jumanne wiki ijayo,”
inaeleza taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo imefafanua kuwa malipo hayo yanafanyika baada ya kukamilika kwa
ukaguzi na uchunguzi uliothibitisha kuwa malalamikaji hakunufaika na
fedha za mkopo na kwamba hao ni watu wawili tofauti.
“Ni
vema kufahamu kuwa makato katika mshahara wa Mwalimu Edwini ambaye ni
mlalamikaji yalisitishwa na alipewa taarifa, lakini kilichokuwa
kinafanywa na Bodi ni kuondoa shaka ya yeye kuwa si mnufaika wa mkopo
kwani kumekuwa na matukio ya watu kulalamika lakini baada ya uchunguzi
inagundulika kuwa wengine ni wadaiwa,” inafafanua taarifa hiyo.
Katika
malamiko yake, Mwalimu Edwini Ndyamukama alinukuliwa na Gazeti la Uhuru
la Januari 3 mwaka huu akieleza kuwa Bodi ya Mikopo walimkata fedha
katika mshahara wake wa mwezi May na June mwaka jana wakati yeye
hakuwahi kukopeshwa na Bodi hiyo.
Mwalimu
Edwini alieleza kuwa baada kuona amekatwa fedha aliandika barua ya
malalamiko na Bodi walisitisha kukata mshahara wake lakini alikuwa bado
hajalipwa fedha zilizokatwa kimakosa.
No comments:
Post a Comment