Trending News>>

Zanzibar Heroes wamkuna Rais wa Zanzibar, atuma salamu za pongezi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepokea kwa furaha kubwa matokeo ya ushindi wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Zanzibar “Zanzibar Heroes” katika mashindano ya  Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ 2017 yanayoendelea nchini Kenya.

Kutokana na matokeo hayo Rais Dk. Shein ametoa pongezi zake za dhati kwa wachezaji wote wa timu ya Zanzibar Heroes pamoja na viongozi wao kwa mafanikio makubwa waliyoiletea Zanzibar hadi kufika fainali.

Dk. Shein alieleza kuwa, kwa hakika ushindi wa Timu ya Zanzibar ni ushindi wa Wazanzibari na Watanzania wote kwa jumla na umeiweka Zanzibar kwenye kiwango kizuri katika ramani ya michezo katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati na nje ya mipaka ya Tanzania.

“Natoa pongezi za dhati kwa wachezaji wote wa “Zanzibar Heroes” pamoja na viongozi wao kwa mafanikio makubwa waliyotuletea hadi kufikia hatua ya fainali ya mashindano hayo”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alieleza matumaini  yake makubwa ya timu ya Zanzibar Heroes kushinda katika mchezo wa fainali kutokana na uwezo mkubwa walioonesha vijana wetu kwenye mashindano hayo.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali na wananchi wote, wako pamoja na timu hiyo pamoja na viongozi wao kwa hali na mali katika kuhakikisha wanarudi na ushindi.

Sambamba na hayo, salamu hizo za pongezi alizozitoa Dk. Shein zilieleza kuwa maandalizi ya kuwapokea na kuwarudisha nyumbani yameshaanza kupitia uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo.

Dk. Shein aliwataka wananchi wote wa Tanzania kuungana  kwa pamoja kuwaombea dua na kuwatakia kila la kheri katika mchezo wa kesho wa fainali watakapocheza na timu ya Harambee Stars ya Kenya.
  
Timu ya Zanzibar Heroes imetinga fainali za michuano hiyo ya Chalenji baada ya kuifunga Uganda mabao 2-1 na kuivua ubingwa katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika jana uwanja wa Moi uliopo Kisumu, Kenya.

Kutokana na matokeo hayo Zanzibar Heroes sasa itacheza fainali za mashindano hayo kwa kuwavaa wenyeji Kenya katika mchezo utakaofanyika kesho Jumaapili.

Kenya ilitinga fainali hizo baada ya kushinda  bao 1-0, dhidi ya Burundi katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza iliyofanyika juzi.

Timu ya Zanzibar ilikuwa katika kundi A, na kundi la Tanzania Bara, Kenya, Libya na Rwanda ambapo ilianza mashindano kwa kuifunga Rwanda mabao 3-1, kabla ya kushinda mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Bara kisha ilitoka suluhu na Kenya na kufungwa bao 1-0 na Libya katika mchezo wa mwisho kuelekea nusu fainali.

Zanzibar Heroes imeandika historia kwa kucheza fainali tangu ilipofanya hivyo mwaka 1995, kuivua Uganda ubingwa lakini pia, imerudia kuifunga tena Uganda kama ilivyofanya mwaka huo 1995 katika fainali ilipotwaa ubingwa kwa kuifunga Uganda bao 1-0 lakini jana iliifunga mabao 2-1.

Mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ yalianza Disemba 2 na yanatarajiwa kumalizika kesho Jumaapili.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

No comments:

Powered by Blogger.