Waziri Mkuu amwagiza Ofisa madini aitishe kikao na wananchi.......Ni baada ya kupokea mabango ya wananchi wakidai kunyanyaswa
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya
Kusini, Bw. Ogesa Charles Tale afike eneo la mgodi wa dhahabu wa Namumgo
na kuitisha kikao cha wananchi leo (Jumapili) saa 4 asubuhi.
“Sasa
hivi natoka kwenda Matambare, twende wote, lakini kesho (leo) saa 4
asubuhi uje hapa Namungo, uitishe mkutano wa hadhara na uwasikilize hawa
wachimbaji wadogo na kisha uniletee maelezo ofisini kwangu,” alisema.
Ametoa
agizo hilo jana mchana (Jumamosi, Desemba 30, 2017), wakati akizungumza
na wakazi wa kijiji cha Namungo, wilayani Ruangwa baada ya kupokea
mabango mawili kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
Waziri Mkuu yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua
miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi katika
wilaya hii.
Waziri
Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano imejikita kusikiliza kero za
wananchi na kuzitafutia ufumbuzi na alipomuuliza afisa huyo kama
ameshawahi kupata nafasi ya kuwasikiliza wachimbaji wadogo, alijibiwa
kwamba hajawahi kufanya hivyo.
“Hawa
ndiyo nguvukazi ya mgodi, hawa ndiyo wanaingia kule chini kuchimba
udongo, hawa ndiyo wanapata machungu ya kazi ya uchimbaji, kwa hiyo uje
uwasikilize na uniletee taarifa kesho mchana,” alisisitiza.
Baada
ya kuyasoma mabango yao, Waziri Mkuu aliwaita wakazi ambao waliyaleta
mabango hayo na kuwataka waeleze kwa undani ni matatizo gani
yanayowakabili. Bango la kwanza lilisema wananchi wananyanyaswa na
viongozi kwa maslahi binafsi ya viongozi na la pili lilisema wamekatazwa
wasiseme matatizo yao kwenye mkutano huo wa Waziri Mkuu.
Mkazi
wa kijiji cha Mtondo, kata ya Nambilanje, Bw. Mussa Omari Kimatilo,
alisema wananyanyaswa na uongozi wa kijiji pamoja na uongozi wa wenye
machimbo ya dhahabu na kwamba wananyimwa uhuru wa kujieleza kila
wanapokutana na viongozi hao.
“Tunanyanyaswa
na uongozi wa machimbo, tunanyanyaswa na uongozi wa kijiji na
tukilalamika hakuna wa kutusikiliza. Tumekaa na Rajani (mmiliki wa
mgodi) amekubali kutulipa lakini wananchi hatuna uhuru wa kujieleza,”
alisema.
Alidai
hata Naibu Waziri wa Madini alipotembelea mgodi huo mapema mwezi huu,
hakupewa fursa ya kukutana na wachimabji wadogo, na badala yake
alipitishwa kijijini hapo na kuingizwa mgodini kisha akaondoka.
Naye
Bahati Mikael, mkazi wa kijiji cha Namungo alisema kumekuwa na
ukiritimba wa kutoa leseni kuhusu mgodi huo na kwamba tangu ilipotolewa
rasmi mwaka 2014, bado hawajalipwa malipo yao.
“Hapa
pana ukiritimba wa kutoa leseni ya uchimbaji. Mwekezaji amekuwa
akichimba kinyemela; tangu mwaka 2006 alikuwa hajapewa leseni hadi mwaka
2014 ndipo alipopewa,” alisema.
Alipoitwa
na Waziri Mkuu atoe ufafanuzi juu ya madai ya wakazi hao, Kaimu Afisa
Madini wa kanda hiyo alisema eneo wanalodai wakazi hao ni la Mzee Kishor
Rajani na inaeleweka hivyo na kwamba miaka ya nyuma walichimba kwa
maelewano tu bila mikataba yoyote.
“Yale
ya nyuma yalishapita kwa sababu hamkuwa na mkataba naye, mlifanya naye
kazi kwa makubaliano ya mdomo tu. Sasa hivi mmeanza kuwekeana mikataba,
zamani alikuwa anachukua asilimia kubwa lakini sasa hivi anachukua
asilimia 17.5 na inayobaki amewaachia ninyi,” alisema Bw. Tale.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara ya jimboni kwake.
No comments:
Post a Comment