WALIODANGANYA RUZUKU YA UCHIMBAJI WATAKIWA KUREJESHA
Serikali imewataka wanufaika wa ruzuku ambao hawakuitumia kama
ilivyokusudiwa warejeshe fedha walizopatiwa mara moja na vyombo vya
ulinzi na usalama vihakikishe waliohusika kuidhinisha wanawajibishwa.
Agizo hilo limetolewa Desemba, 12, 2017 na Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo Mkoani Singida wakati wa ziara yake ya kutembelea
Migodi ya Dhahabu kwa ajili ya kujionea shughuli zinazoendelea na
kuzungumza na wachimbaji.
“Aliyenufaika na ruzuku na hakufanya lolote, arejeshe mara moja fedha
hiyo na aliyehusika kuwapatia ruzuku watu hawa hali yakuwa anaelewa
hawakuwa na dhamira ya kuendeleza uchimbaji nae achukuliwe hatua,”
aliagiza Nyongo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto aliyenyoosha
mkono) akielekeza jambo alipotembelea Mgodi wa Dhahabu wa
Mwandami Small Scale Mine uliopo katika Kijiji cha Sambaru, Kata ya
Mang’onyi Wilayani Ikungi.
Agizo hilo linafuatia malalamiko ya wachimbaji wadogo ambao
hawakunufaika na mpango huo wa ruzuku ambapo walimueleza
kwamba wapo baadhi ya watu wasiostahili lakini walipatiwa ruzuku.
Naibu Waziri Nyongo alisema anampongeza Rais John Magufuli kwa
uamuzi wake wa kusimamisha utoaji wa ruzuku kwani imeshindwa
kufikia matarajio yaliyokusudiwa.
Alisema Serikali ilisimamisha utoaji wa ruzuku kwa wachimbaji wadogo
wa madini nchini baada ya kubaini kwamba imeshindwa kuleta
mafanikio yaliyokusudiwa.
Nyongo alisema dhamira ya Serikali ya kutoa ruzuku ilikuwa ni
kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini nchini wanaweza
kuendeleza machimbo yao kwa kufanya shughuli zenye tija kwao na
Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo alisema dhamira hiyo haikuzaa matunda yaliyokuwa
yamekusudiwa kwani imedhihirika kwamba ruzuku iliyotolewa
haikuwanufaisha walengwa kama ilivyotarajiwa badala yake ilinufaisha
watu wachache tofauti na ulivyokuwa mpango mzima wa utoaji wake.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akitazama
mtambo wa kusaga mawe yenye Madini ya Dhahabu uliopo kwenye
Mgodi wa Mzaki na Wenzake uliopo katika Kijiji cha Mwau, Wilayani
Ikungi. Kulia ni Mmoja wa Wamiliki wa mgodi huo, Kasirate Mzaki.
“Wapo wachimbaji wachache ambao walifanikiwa kupata ruzuku na
waliweza kuendeleza migodi; japo hawa ni wachache tofauti na malengo
ya Serikali,” alisema Naibu Waziri Nyongo.
Mbali na hilo, alisema baadhi ya wachimbaji wadogo walipewa ruzuku
na walichimba lakini hawakufanikiwa kwani walichimba kwa kubahatisha
bila kuwa na elimu ya kutosha ya kutambua uwepo wa mashapo katika
maeneo yao.
Kwa kuliona hilo, Nyongo alisema Serikali ipo katika majadiliano na
Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini kuona namna
ambavyo wanaweza kuwa na uchimbaji wenye tija.
Alieleza kwamba Wizara ya Madini kwa kushirikiana na wachimbaji
wadogo katika umoja wao wameona ipo haja ya kuwasaidia kufanya
utafiti kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Shirika la Madini la
Taifa (STAMICO) ili waweze kutambua maeneo yenye mashapo na
hivyo kuepukana na uchimbaji wa kubahatisha.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) alipotembelea
Mgodi wa Dhahabu wa Mwandami Small Scale Mine unaomilikiwa na
Yusufu Mwandami (kushoto) uliopo katika Kijiji cha Sambaru, Kata ya
Mang’onyi Wilayani Ikungi.
“Wachimbaji wengi wanafanya uchimbaji kwa kubahatisha na ndiyo
maana wapo wengine ambao wanakimbilia kwenye imani za kishirikina.
Hii yote ni kukosa elimu, ya utambuzi wa maeneo sahihi,” alisema.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji
Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina alisema wanaunga
mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha wanakuwa na uchimbaji
wenye tija.
Hata hivyo alisema changamoto inayowakabili wachimbaji wadogo walio
wengi ni ukosefu wa elimu ya utambuzi wa maeneo sahihi yaliyo na
mashapo na kwamba msaada wa Serikali wa kufanya utafiti utawasaidia
kufanya uchimbaji wenye faida.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini
Tanzania (FEMATA), John Bina (kulia) akizungumza na Wachimbaji
Wadogo wa Madini ya Dhahabu kutoka Wilaya ya Ikungi na Manyoni
Mkoani Singida (hawapo pichani), wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kutoka kushoto) katika Kijiji cha
Londoni.
Naibu Waziri wa Madini akizungumza na Wachimbaji Wadogo wa
Madini ya Dhahabu kutoka Wilaya ya Ikungi na Manyoni Mkoani Singida
(hawapo pichani), wakati wa ziara yake katika Kijiji cha Londoni.
Baadhi ya Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Dhahabu kutoka Wilaya ya
Ikungi na Manyoni Mkoani Singida wakimsikiliza Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), wakati wa ziara yake katika
Kijiji cha Londoni.
No comments:
Post a Comment