Viongozi wa umma watakiwa kukabidhi orodha ya mali zao kabla ya Desemba 31
Kamishna
wa Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu
Harold Nsekela amewahimiza Viongozi wa Umma kukamilisha taratibu za
ujazaji wa fomu za tamko la rasilimali na madeni kabla ya Disemba 31
mwaka huu.
Ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es
Salaam alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma inayomtaka kiongozi wa umma kupeleka tamko
kwa maandishi lililo katika hati rasmi linaloorodhesha mali au
rasilimali za kiongozi na familia yake kwa Kamishna wa Maadili kila
mwisho wa mwaka.
Jaji Mstaafu Nsekela amesema kuwa fomu
za tamko hilo zinapatikana kwenye tovuti ya Sekretarieti ya maadili
ambayo ni www.ethicssecretariat.go.tz hivyo ametoa wito kwa viongozi
ambao hadi sasa hawajapata fomu kutumia tovuti hiyo kupata fomu kwa
urahisi.
“Kwa kuzingatia kifungu cha 9 (1)
(a) na (c) cha Sheria na Maadili ya Viongozi wa Umma, viongozi wapya
wanaochaguliwa au kuteuliwa wanatakiwa kujaza fomu hizi ndani ya siku
thelathini baada ya kupewa wadhifa fulani pia anapofika mwisho wa
kutumikia wadhifa huo anapaswa kujaza fomu na kuzirejesha katika ofisi
yetu,” alisema Jaji Mstaafu Nsekela.
Jaji Mstaafu Nsekela amefafanua kuwa
fomu hizo zinatakiwa kuwasilishwa katika Ofisi ya Sekretarieti ya
Maadili ya viongozi wa Umma zilizopo Jijini Dar es Salaam au katika
ofisi zao za Kanda zilizopo katika Mikoa ya Dodoma, Mwanza, Arusha,
Mtwara, Tabora, Pwani na Mbeya.
Kwa upande wake Afisa Sheria Mkuu wa
Sekretarieti hiyo, Filotheus Manula amesema kuwa kujaza fomu hizo ni
takwa la kikatiba hivyo Viongozi wa Umma wahakikishe wanajaza fomu hizo
bila kudanganya.
“Ni kosa kwa mujibu wa Kifungu cha
15(c) cha Sheria za Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kiongozi kushindwa
kutoa tamko bila sababu ya msingi kwani sheria hizi hazimzuii kiongozi
kumiliki au kuwa na mali nyingi bali mali hizo zinatakiwa kutolewa
maelezo ya chanzo cha upatikanaji wake,” alisema Manula.
Aidha, Manula amefafanua kuwa kosa hilo
linaweza kumpelekea muhusika kuonywa au kupewa adhabu ya kushushwa
cheo, kusimamishwa, kufukuzwa kazi pamoja na kupelekwa Mahakamani.
Vile vile Manula amesema kuwa kwa sasa
hali ya uadilifu kwa Viongozi wa Umma inaridhisha kwani ukiukwaji wa
maadili umepungua kwa kiasi kikubwa.
Na Jacquiline Mrisho
No comments:
Post a Comment