Kilimo Bora cha Alizeti
MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA WAKATI WA UZALISHAJI
Kuchagua aina bora ya mbegu
- Chagua aina bora ya mbegu inayovumilia magonjwa, wadudu, inayotoa mazao mengi na kiwango kikubwa cha mafuta.
- Vilevile chagua aina ya mbegu ambayo hukomaa kwa wakati mmoja ili kurahisisha uvunaji.
KUWEKA MBOLEA
Rutubisha udongo kwa kutumia mbolea za mboji na samadi ili kupata mazao mengi na bora.
KUDHIBITI WADUDU NA MAGONJWA
Alizeti hushambuliwa na magonjwa ya majani, mizizi na masuke ambayo husababisha upungufu wa mavuno. Hivyo ni muhimu kuyadhibiti ili kupata mavuno mengi na bora. Pia ndege hupunguza mavuno kwa kiasi cha asilimia 50 au zaidi. Njia ya kudhibiti ndege ni kwa kuwafukuza na kupanda mbegu zinazokomaa mapema.
MAANDALIZI KABLA YA KUVUNA;
Kagua shamba kuona kama alizeti imekomaa. Alizeti hukomaa kati ya miezi minne hadi sita tangu kupanda. Wakati huo punje huwa na unyevu wa asilimia 25. Ni muhimu kuvuna alizeti mapema ili kuepuka mashambulizi ya panya, mchwa na ndege waharibifu.
DALILI ZA ALIZETI ILIYOKOMAA
- Suke hubadilika rangi kutoka manjano na kuelekea kuwa nyeusi.
- Viuwa vya pembeni mwa suke hunyauka na hubadilika kutoka rangi ya manjano na kuwa ya kahawia.
UVUNAJI, UKAUSHAJI NA UBEBAJI
Vifaa vya kuvunia na kubebea kutoka shambani
- Kisu
- Vikapu
- Magunia
- Matenga Vifaa vya kukaushia
- Maturubai
- Mikeka
- Kichanja bora Vyombo vya usafiri kutoka shambani
- Matoroli
- Matela ya matrekta
- Mikokoteni ya kukokotwa na wanyama
- Magari KUVUNA Alizeti huvunwa kwa kutumia mikono ambapo suke hukatwa kwa kutumia kisu. Pia mashine (combine harvester) hutumika kuvunia alizeti katika nchi zinazolima alizeti kwa wingi. Masuke ya alizeti huwekwa kwenye vikapu ambavyo hutumika kusomba alizeti ndani ya shamba. Kisha alizeti hufungashwa kwenye magunia na kusafirishwa hadi nyumbani tayari kwa kukausha.
KUKAUSHA
Kuna hatua mbili za kukausha alizeti; kukausha masuke na kukausha mbegu za alizeti. Kukausha masuke
- Masuke hutandazwa kwenye kichanja bora katika kina kisichozidi sentimita 30 ili yaweze kukauka vizuri.
- Vilevile huweza kutandazwa kwenye maturubai, mikeka au sakafu safi.
- Lengo la hatua hii ni kukausha masuke ya alizeti ili kurahisisha upuraji. KUPURA Upuraji hufanyika baada ya kuhakikisha kuwa masuke ya alizeti yamekauka vizuri. Masuke ya alizeti hupurwa kwa kutumia mikono ambapo mbegu hutenganishwa kwa kupiga masuke taratibu kutumia mti. Ni muhimu kupiga masuke taratibu ili kuepuka kupasua mbegu
- Pura kwenye kichanja bora, maturubai au mikeka.
KUKAUSHA MBEGU
- Mbegu za alizeti hukaushwa juani kwa kutandazwa kwenye vichanja bora, maturubai, mikeka au sakafu safi.
- Tandaza mbegu katika kina kisichozidi sentimita 4 ili ziweze kukauka vizuri.
- Lengo la hatua hii ni kukausha mbegu baada ya kupura ili kufikia kiwango cha unyevu kinachotakiwa kwa hifadhi salama ambacho ni asilimia 8.
JINSI YA KUTAMBUA MBEGU ZILIZOKAUKA VIZURI
Kufikicha mbegu
- Mbegu zilizokauka maganda yake hutoka kwa urahisi zinapofikichwa. Kumimina kwenye chombo kama debe
- Mbegu zilizokauka hutoa mlio mkali zinapomiminwa kwenye vyombo hivyo.
- Mbegu zilizokauka hung’ara Kutumia kipima unyevu.
- Mbegu zilizokauka vizuri kipimo huonyesha asilimia 8
KUPEPETA NA KUPEMBUA
Kupepeta na kupembua hufanyika ili kuondoa takataka kama vile mawe,
wadudu, mapepe, mbegu zilizooza au kupasuka. Mbegu za alizeti hupepetwa
kwa kutumia ungo au mashine zinazoendeshwa kwa mkono, injini au umeme.
Mashine hizi zina uwezo wa kupepeta na kupembua kilo 60 hadi 350 kwa saa
kutegemea aina ya mashine na ukubwa wa mashine yenyewe
KUHIFADHI
Alizeti iliyopurwa huhifadhiwa katika hali ya kichele kwenye maghala
bora, yaani vihenge, sailo au bini. Alizeti ya kuhifadhi kwenye maghala
ya nyumba ifungashwe kwenye magunia na ipangwe kwenye chaga kwa
kupishanisha. Ili kurahisisha kazi ya kukagua ghala, acha nafasi ya mita
moja kutoka kwenye ukuta. Ziba sehemu zote za ghala ili kuzuia panya
kuingia.
Panya hupenda sana kula punje za alizeti, na husababisha upungufu mkubwa
wa punje ambao husababisha upotevu wa asilimia 30 kwa kipindi cha miezi
mitatu ya hifadhi. Asilimia ya upotevu inaweza kuwa kubwa zaidi
kutegemea idadi ya panya na upatikanaji wa vyakula vingine kwa wakati
huo. Matumizi ya Mbegu za Alizeti Mbegu za alizeti hasa zenye mistari
zinaweza kuliwa baada ya kukaangwa au kukaushwa. Pia zinatumika katika
utengenezaji wa mikate. Mbegu za alizeti husindikwa kupata bidhaa ya
mafuta.
KUSINDIKA MBEGU ZA ALIZETI KUPATA MAFUTA
- Vifaa
- Mashine ya kukamua mafuta
- Chujio safi
- Ndoo
- Vifungashio
- Sufuria
- Mizani Malighafi
- Mbegu za alizeti
- Maji
- Chumvi
NJIA YA KUKAMUA MAFUTA
- Chagua mbegu bora za alizeti
- Zianike kwenye jua kwa muda wa saa 1 hadi 2
- Weka kwenye mashine ya kukamulia ya daraja au Ram
- Kamua mafuta
- Chuja mafuta kwa kitambaa au chujio safi
- Pima mafuta yaliyokamuliwa.
- Ongeza maji na chumvi. Katika lita 10 za mafuta weka lita moja ya maji na gramu 200 za chumvi. • Weka mafuta kwenye chombo cha kuchemshia (sufuria)
- Chemsha hadi maji yote yaishe
- Sauti ya kuchemka ikiisha ni dalili kuwa maji yamekwisha.
- Ipua, acha yapoe, kisha chuja kwa kitambaa safi au chujio
- Fungasha kwenye vyombo safi na vikavu na vyenye mifuniko
- Weka lakiri na lebo
- Hifadhi kwenye sehemu safi, kavu na yenye mwanga hafifu.
MATUMIZI
Mafuta hutumika katika mapishi mbalimbali na yana virutubishi vifuatavyo: - Mafuta gramu 100 Nguvu kilokalori 900.
No comments:
Post a Comment