Trending News>>

UVCCM Mmemsikia Rais Magufuli?


UVCCM wakiendelea na kikao.
KAMA ilivyo kawaida yangu napenda tena kumshukuru Mungu kwa kuendelea kunipigania katika kutimiza majukumu yangu ya kila siku.

Katika hilo nasema asante Bwana Mungu kwani wewe ndiye mwenye uwezo wa kila kitu kwa kuendelea kunipa pumzi ninayovuta sasa.

Baada ya kusema hivyo napenda kuzungumzia suala la rushwa ambalo Rais Dk. John Magufuli alililamikia ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wiki iliyopita.
Itakumbukwa kuwa wakati akifungua mkutano mkuu wa umoja huo nchini Dodoma, Rais Magufuli aliweka wazi kuwa umoja huo umejaa rushwa na kwamba hilo ni tatizo kubwa.

Alikumbusha vijana kuwa UVCCM ya sasa ni tofauti na ya miaka iliyopita na kuwataka viongozi wapya kuujenga upya umoja huo ili kuondoa vitendo vya rushwa na kuimarisha uzalendo.
Wakati Rais Magufuli akisema hivyo, Mwenyekiti wa zamani wa UVCCM, Sadifa Khamis alikuwa amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa tuhuma za rushwa.

Kauli ya Rais Magufuli ilionekana kugusa hisia za viongozi wa umoja huo ndiyo maana mwenyekiti mpya wa UVCCM, Kheri James alikuwa na haya ya kusema;
“Nataka itengenezwe hotuba ya mwenyekiti wetu wa chama (Rais Magufuli), kila alichotueleza tukipate na isambazwe hadi ngazi za chini kwa viongozi wetu ili ifanyiwe kazi.
“Kama kuna kazi kubwa tuliopewa ni kwenda kudhibiti rushwa kwenye ngazi zote, na sisi kazi hii tutaifanya,” alisema James.

Kusema na kutenda ni jambo jingine, lakini niseme tu hapa kwamba UVCCM chini ya uongozi inatakiwa ijisafishe na kufanya kazi kwa kasi ya Rais Magufuli.
Tunaamini kwamba endapo umoja huo utakuwa imara bila shaka uongozi wa nchi utakuwa pia mzuri. Hii maana yake ni kwamba bila uongozi imara wa UVCCM hakuna CCM imara.

Kwa maana hiyo tunatarajia kuona uongozi imara wa umoja huo ukifanya kila linalowezekana kuhakikisha rushwa inafutika katika taasisi hiyo, vinginevyo watakuwa wanamkejeli rais na vijana wa Kitanzania.

UVCCM inatakiwa kuwa mfano mzuri kwa kila nyanja. Hii ikiwa na maana kuwa kuanzia kwenye shughuli za utendaji wa kila siku.
Kama umoja huo utakuwa mfano mzuri kusimamia shughuli mbalimbali za uzalishaji maana yake utakuwa chachu kwa vijana.

Lakini ukilegelega na kufanya mambo ovyo ovyo kusema kweli utaonesha taswira mbaya kwa vijana na hata Watanzania wengine kwa ujumla.
Ndiyo maana nasisitiza kuwa ushauri wa Rais Magufuli unatakiwa

kuzingatiwa na kufanyiwa kazi kwa ustawi wa umoja na nchi kwa ujumla.
Hili litawezekana kwa namna gani? Kwanza, ni lazima umoja huo uwe na viongozi wenye maadili ili mambo mengine yaende vizuri.
Kama kiongozi hana maadili ni vigumu kusimamia wengine vizuri. Ni vigumu kupiga vita rushwa na matendo mengine maovu kama kiongozi hana moyo na nia ya kupiga vita rushwa na ufisadi.
Kwa sababu hiyo, Rais Magufuli ni kana kwamba ametupa bomu la mkono kwa UVCCM, sasa kazi ipo kwa viongozi husika lisiwalipukie.

Ndiyo kusema mwenyekiti mpya ana kazi ya kumthibitishia rais kwamba kweli amedhamiria kujenga umoja mpya usio na rushwa, ufisadi wala mmomonyoko wa maadili.
Umoja huo unatakiwa pia kuhakikisha fedha zinazopatikana katika vitega uchumi vyake ili vijulikane badala ya kuendeshwa tu kinyemela.

Ni kazi ya uongozi mpya kutambua mali zake ziko wapi na fedha zinazopatikana kwenye vitega uchumi wake vinaishia wapi.
Lakini pia, kuhakikisha unapitia historia vizuri ili kujua umoja wa zamani ulikuwaje na wa leo upo sahihi ama kuna mahali umeteleza.
Hayo na mengine mengi yakifanyiwa kazi kwa kina yatasaidia kujenga taswira nzuri ya UVCCM machoni mwa jamii ya Kitanzania.

Jambo la msingi kwa sasa ni uongozi wa umoja huo kufanyakazi kwa vitendo ili kuleta matunda chanya kwa ustawi wa umoja na wanachama.
Ni imani yangu kuwa yote aliyosema Rais Magufuli endapo yatafanyiwa kazi kwa umakini itasaidia kuondoa dosari zinazosemwa.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
Napasua Jibu na Eric Shigongo, Dar es Salaam

No comments:

Powered by Blogger.