Ushindi wa CCM watenguliwa na Mahakama
Mahakama ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara imetengua ushindi wa CCM wa
nafasi ya mwenyekiti wa Kitongoji cha Sola kilichopo Kata ya Mutuka na
kuamuru uchaguzi urudiwe.
Mgombea wa CCM alipita bila kupingwa baada ya mgombea wa Chadema kuenguliwa katika mchakato wa uchaguzi.
Hakimu John Shao akitoa hukumu ya kesi namba 1/2017 jana Jumanne Desemba 12,2017ameamuru uchaguzi ufanyike upya kwa nafasi hiyo.
Kesi hiyo ilifunguliwa na mgombea uenyekiti wa kitongoji hicho
(Chadema), Vincent Slaa akipinga kuenguliwa na kamati ya rufaa ya
uchaguzi ya wilaya hiyo. Aliwakilishwa na wakili Tadey Lister.
Hakimu Shao amesema Mahakama inakubaliana na pingamizi lililowekwa na
Slaa kwamba alienguliwa kwenye mchakato wa uchaguzi bila sababu za
msingi, hivyo Sagwale wa CCM akapitishwa bila kupingwa kwa nafasi ya
mwenyekiti wa kitongoji.
Amesema Slaa aliondolewa kwenye mchakato wa uchaguzi uliofanyika Aprili 29,2017 na kamati ya rufaa ya uchaguzi Wilaya ya Babati.
Hakimu Shao ameamuru uchaguzi wa nafasi hiyo urudiwe na upande wa wadaiwa unapaswa kulipa gharama za kuendesha kesi hiyo.
"Kamati ya rufaa ya uchaguzi ya Wilaya ya Babati haikutenda haki
ilipoondoa jina la Slaa kwenye uchaguzi, hivyo Mahakama inatengua nafasi
ya Sagwale aliyepitishwa bila kupingwa na kuamuru uchaguzi ufanyike
upya," alisema hakimu Shao.
Wadaiwa wengine kwenye kesi hiyo ni kamati ya rufaa ya uchaguzi,
msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa kata ya Mutuka na msimamizi wa
uchaguzi wa jimbo.
Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul ametoa shukrani kwa
Mahakama kwa kutenda haki kwa kuwa mgombea wa chama hicho aliondolewa
kwenye mchakato huo kwa kuonewa.
"Mgombea wa CCM alipitishwa bila kupingwa sasa turudi uwanjani ili
nafasi hiyo ipate mwenyewe kwa jasho na kwa halali kupitia kura za
wananchi," amesema Gekul.
Aliyekuwa mwenyekiti wa kitongoji hicho, Sagwale alisema wananchi wa
eneo hilo wana imani naye kwa kuwa muda mfupi aliowaongoza wamempa
ushirikiano wa kutosha.
No comments:
Post a Comment