Ukimfanyia Haya Mwanaume Hakuachi Abadani!!
Kama ulikuwa na ‘mushikeli’ za hapa na pale basi wafufue upya penzi lao. Mtafakari upya kuhusu safari yenu, wapi mlikosea? Mliweka mikakati ya kufanya kwa mwaka 2017 na haijatimia, ni vyema mkaweka mikakati upya kwa mwaka 2018 ili muweze kufikia hatua nzuri na kubwa mliyoipanga. Hakuna linaloshindikana. Kikubwa ni kupanga na kutekeleza mipango mliyojiwekea. Wengi wetu tumekuwa tukishindwa kufikia malengo kwa sababu tunaishia kwenye kupanga.
Hatuthubutu. Kutothubutu ndilo tatizo kubwa. Mathalan, mmepanga hadi mwezi fulani muwe mmevalishana pete, kweli mfanye hivyo kwa kujua mahitahi ya pete ni nini? Vivyo hivyo kama mmeshavalishana, nini kinafuata? Kinahitaji nini ili kiweze kufanyika? Yale mahitaji ndio mnapaswa kuyashughulikia kwa haraka bila kupoteza muda. Naamini mkiishi kwa kusimamia mikakati na muda, hakika mtafikia malengo yenu.
Muhimu ni kuthubutu, usiogope
anza kutekeleza jambo fulani kisha mengine yatajileta yenyewe kwenye mstari. Nikirudi kwenye mada yangu, wanawake wengi wamekuwa wakishindwa kuwasoma vizuri wanaume na kujikuta wakitofautiana na wanaume wao. Mwanaume anapenda kusikilizwa. Kushauriwa kwa kutumia lugha ya staha.
Hata kama unajua amekosea, usimshushe katika kumkosoa. Tumia lugha rafiki katika muda muafaka (akiwa hana hasira) na hakika atakuelewa. Mbembeleze. Mwanaume ukimbeleza, ukampokea kwa bashasha anapotoka kwenye mihangaiko yake, ukampa pole na kumkaribisha nyumbani basi atajisikia mwenye thamani sana. Mpe kipaumbele yeye katika mambo mengi ya msingi. Muoneshe kwamba yeye ndio baba wa familia.
Yeye ndio mwenye maamuzi ya mwisho ndani ya familia, atakupenda sana. Sina maana kwamba mwanamke asiwe mtu wa maamuzi, au asiwe na msimamo wake katika jambo fulani lakini kimsingi mwanaume ni dhaifu kwa mwanamke. Unapomjali, unapomthamini hata kama una msimamo wako katika jambo fulani, mueleze katika muda huo uone kama atapindua. Kiulaini kabisa atakubaliana na wewe. Mwanaume hapendi mabishano. Unachotakiwa kufanya ni kuyaepuka kwa namna yoyote. Hata kama unaona hayupo sahihi, mvutie kasi. Tafuta muda rafiki, utamueleza akiwa na furaha na wala hataleta ubishi.
Mwanaume hapendi mwanamke anayeongea sana. Anapenda kusikilizwa zaidi. Anapenda kuheshimika, mheshimu kweli kweli wala hakuna atakayekucheka eti kwa nini unamheshimu mumeo. Usipomheshimu yeye unataka umheshimu nani? Mheshimu uone namna ambavyo mtaishi vizuri ndani, kwanza naye atakuheshimu. Atakusikiliza, atakupa mahitaji yote kadiri ya uwezo wake. Mwanaume hapendi kuonekana dhaifu. Tumia ufundi wako kumfanya ajishushe.
Kuna wakati atakuwa dhaifu bila hata kumlazimisha. Ataelewa kile alichokifanya si sahihi na ulichokuwa nacho wewe ndio sahihi. Cha mwisho ni faragha, wanawake wengi wanajisahau. Pamoja na mambo mengine ya kuonesha upendo, faragha pia ni eneo muhimu. Mwanamke fanya kila unalofanya lakini hakikisha unamridhisha mwenzi wako. Inaelezwa kuwa wanaume ni wadhaifu sana katika kuhimili matamanio tofauti na wanawake. Jitahidi kumridhisha, achana na habari za nimechoka. Mridhishe asipate mwanya wa kutamani wengine. Niwatakie sikukuu njema!
No comments:
Post a Comment