Tigo mtandao Ghali zaidi kupiga / sms
Ripoti ya robo ya tatu ya mwaka huu ya TCRA inabainisha kuwa wateja wa mtandao huo hulipa zaidi kufanya mawasiliano kwa namna zote; iwe kupiga au kutuma sms ndani au nje ya mtandao au kufanya hivyo nje ya nchi.
Ripoti ya TCRA kwa robo iliyoishia Septemba inaonyesha wateja wa Tigo hutozwa Sh360 kupiga simu kwenda kwa wenzao wanaotumia mtandao huo kwa dakika moja, hivyo kuufanya kuwa ghali zaidi ikilinganishwa na mitandao mingine nchini.
Tozo hiyo ipo juu ya wastani wa gharama za kupiga simu ambazo ni Sh278 kwa dakika.
Kampuni inayofuata ni Vodacom ambayo wateja wake wanalipa Sh270 kwa dakika; ikifuata Halotel kwa gharama ya Sh228 na Airtel wakilipa Sh219.
Ripoti ya TCRA inaonyesha, wateja wa TTCL, Zantel na Benson (Smart) ndio wanaolipa gharama ndogo zaidi kuwasiliana.
Wateja wa TTCL wanatozwa Sh154 kwa kila dakika; Zantel (Sh157) na Benson (Sh60) kupiga simu kwa muda huo.
Tigo pia ni ghali kwa kupiga simu kwenda mitandao mingine. Ripoti inaonyesha kampuni hiyo hutoza Sh480 kwa dakika - kiwango ambacho ni kikubwa kuliko wastani uliopo.
Takwimu zinaonyesha wastani wa gharama za kupiga simu kwenda mtandao mwingine ni Sh365 kwa kila dakika.
Kama ilivyo kwa gharama za ndani ya mtandao, kampuni nyingine hutoza chini ya wastani. Ripoti inaonyesha wateja wa Airtel hulipa Sh361 ilhali wa Vodacom wakilipa Sh330 na TTCL Sh274.
Wanaotumia mtandao wa Benson hulipa kidogo zaidi kama ilivyo kupiga ndani ya mtandao. Wao hutozwa Sh150 wakifuatiwa na Halotel wanaolipa Sh228 na Zantel Sh249.
Afrika Mashariki
Kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kiwango kinachotozwa na Tigo kipo chini kidogo kwa kuwa hutoza Sh1,022 kwa dakika kulinganisha na Halotel wanaotoza Sh1,033 na Zantel Sh1,020.
Kampuni hizo tatu zinatoza gharama kubwa kuliko wastani wa kupiga simu katika nchi za EAC ambao ni Sh795.
Zinazotoza chini ya wastani huo ni Airtel inayotoza Sh750; Vodacom (Sh719); TTCL (Sh650) na Benson (Sh198).
Kwa watumiaji wanaopiga simu nje ya Afrika Mashariki, wateja wa Tigo hutozwa gharama kubwa ya Sh1,737 kulinganisha na Airtel (Sh1,520), Halotel (Sh1,330), Vodacom (Sh1,090), Benson (Sh868) na TTCL (Sh600). TCRA inaonyesha wastani wa gharama hizo ni Sh1,355. Ripoti ya TCRA inaonyesha wastani wa gharama za kutuma sms ni Sh59 lakini Tigo inaongoza kwa kutoza Sh70 ikifuata Zantel Sh65.
Mitandao inayotoza gharama ndogo chini ya wastani ni Vodacom (Sh51), Airtel (Sh50), TTCL (Sh47), Benson (Sh40) na Halotel (Sh30). Hata kutuma sms kimataifa, Tigo inaongoza kwa gharama ikitoza Sh215 ikifuatiwa na Airtel (Sh156), Vodacom (Sh153), Benson (Sh145), Zantel (Sh138) na TTCL (Sh117). Halotel ndiyo yenye gharama ndogo zaidi, hutoza Sh95.
Mpaka Septemba, Vodacom inaongoza kwa wingi wa wateja ikiwa nao 12.8 milioni (sawa na asilimia 32) ikifuatiwa na Tigo yenye wateja 11 milioni (sawa na asilimia 28)na Airtel yenye wateja 10.6 milioni (sawa na asilimia 27).
Halotel inashika nafasi ya nne ikiwa na wateja 3.7 milioni ikifuatiwa na Zantel yenye wateja 900,000; Benson (Smart) yenye 500,000 na TTCL 300,000.
No comments:
Post a Comment