TCRA Yatangaza Bei Mpya Za Kupiga Simu, Yaitoza Startimes Faini
MAMLAKA
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetangaza bei mpya za mwingiliano wa
mitandao ya simu hapa nchini kwa dakika moja kuanzia Januari mosi,
mwakani huku ikizitaka kampuni za mitandao kuongeza dakika za maongezi
kwa wateja wao.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James
Kiliba, alisema uamuzi wa Serikali kutoa viwango vipya vitakavyodumu
kwa miaka mitano (2018/2022), ni baada ya kufanya utafiti wa gharama za
kampuni –fanisi (efficient operator) za uendeshaji wa mitandao ya simu
namba tano wa mwaka huu.
Alisema
mbali na kufanya utafiti, pia walikusanya maoni ya wadau husika kama
ilivyoelekezwa katika kifungu namba 18(2) cha sheria ya namba 12 ya TCRA
ya mwaka 2003 na kuunda jopo la wataalamu la kupitia maoni ya wadau juu
ya gharama za mwigiliano zilizopendekezwa na TCRA.
Kiliba
alisema kuanzia Januari mosi, gharama ya mwigiliano kwa dakika moja
itakuwa Sh 15.60, mwaka 2019 itakuwa Sh 10.40, mwaka 2020 itakuwa Sh
5.20, mwaka 2012 itakuwa Sh 2.60 na mwaka 2022 itakuwa Sh 2.00.
Alisema
Serikali imeamua kushusha viwango hivyo zaidi tofauti na miaka mitano
iliyopita ambapo kwa mwaka 2013 ilikuwa ni Sh 34.92, mwaka 2014 ilikuwa
ni Sh 32.40, mwaka 2015 ilikuwa ni Sh 30.54, mwaka 2016 ilikuwa ni Sh
28.57 na mwaka 2017 ilikuwa ni Sh 26.96.
Kiliba
alisema kabla ya viwango hivyo, Serikali ilitoa ruhusa kwa wenye
kampuni za mitandao ili kukaa na kupendekeza bei lakini walishindwa
kuelewana kutokana na mvutano wa biashara yao ndipo ilipoamua kufuata
sheria na kufikia kutangaza bei hizo.
“Kushuka
kwa gharama za mwingiliano kutasababisha ongezeko la dakika za maongezi
na hivyo kuongezeka kwa mapato ya watoa huduma na ya Serikali kutokana
na ongezeko la matumizi ya huduma mbalimbali za mawasiliano.
“Kama
TCRA inatarajia kwamba, kupungua kwa gharama za mwingiliano
kutasababisha kushuka kwa gharama za kupiga simu kwenda mitandao mingine
na hivyo kupunguza ulazima wa wateja kuwa na laini zaidi ya moja kwa
kuhofia gharama kubwa kwenda mitandao mingine.
“Awali
nimewaeleza laini zinazotumika hadi sasa zimefikia zaidi ya milioni 40,
hivyo kuongezeka kwa matumizi ya huduma za mawasiliano kutawezesha na
kuongeza ufanisi katika shughuli za sekta nyingine kiuchumi na kijamii,
wito wetu kama mamlaka ni kuwataka watoa huduma kuzingatia viwango
vipya, vinginevyo sheria zitachukua mkondo wake,” alisema.
Pia
alisema gharama zilizotolewa ni bei za jumla ambazo kampuni za simu
hulipana ili kufidia gharama ya kupokea simu inayotoka mtandao mwingine
na kuifikisha kwa mteja aliye ndani ya mtandao unaopigwa na viwango
hivyo si bei ya rejereja anayotozwa mteja anapopiga simu.
IDADI YA SIMU ZA MIKONONI, MEZANI
Pia
alisema Tanzania imeendelea kupata mafanikio katika sekta ya
mawasiliano ambapo idadi ya watoa huduma na watumiaji imeendelea
kuongezeka na kukuwa kwa biashara na ujasiriamali.
“Kwa
upande wa mawasiliano ya simu, idadi ya simu za mezani imeongezeka
kutoka 16,238 mwaka 1961 hadi 127,976 Septemba, mwaka huu, kila mwaka
kulikuwa na ongezeko fulani lakini kasi ipo juu kwa upande wa watumiaji
wa simu za mkononi kwa sababu zimeongezeka kutoka laini 2,963,737 kwa
mwaka 2005 hadi laini 40,002,364 kufikia Septemba, mwaka huu.
“Katika
upande wa simu za kufanya miamala za kifedha, huduma hii nayo imekuwa
tangu mwaka 2008 kwa sababu ilikuwa ni kampuni moja tu lakini hadi leo
zimefikia kampuni sita ambazo ni Airtel, Tigo, Halotel, TTCL, Vodacom na
Zantel, watumiaji wa miamala walikuwa 17,639,349 kwa mwaka 2015, lakini
hadi Septemba, mwaka huu wamefikia 21,611,855.
“Watumiaji
wa intaneti wameongezeka kwa kasi kutoka 1,681,012 kwa mwaka 2005
lakini hadi Septemba, mwaka huu wamefikia 22,841,903, hili ni ongezeko
kubwa la muda mfupi. Serikali tunaendelea kuboresha miundombinu ili
kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia,” alisema.
Kuhusu
mitandao ya kijamii, alisema kuna watu wanaitumia isivyo kwa kuweka
vitu ambavyo si vyake kweli na vingine vinakwenda kinyume na maadili ya
Watanzania ikiwamo picha za utupu na aliliomba Jeshi la Polisi kuwa
makini kwa kuwakamata wahusika.
“Sisi
TCRA tunatoa miongozo na kudhibiti watumiaji lakini hatuwezi kukamata
ila tunasaidiana na polisi kuwakamata wahusika, hivyo kila mnachokiona
kinakwenda kinyume huwa tunahusika na wengine wamekamatwa, si kwamba
kila kitu tutakisema hatua zilizofikiwa, tunaomba ushirikiano hasa
waandishi wa habari,” alisema.
FAINI STAR TIMES
Akizungumzia
faini za chaneli za bure za televisheni, alisema baadhi ya kampuni
zenye ving’amuzi zimekuwa zikikiuka kanuni ya 14 (2)(a) ya mwaka 2011
kwa kushindwa kuonyesha chaneli tano za bure huku zikiwatoza wateja wao.
Alisema
baada ya ufuatiliaji wa kampuni hizo, TCRA ilibaini Kampuni ya Star
Media Tanzania Ltd inayomiliki king’amuzi cha Star Times haionyeshi
chaneli hizo huku ikiwatoza watazamaji wake ndipo Desemba 22, mwaka huu
Serikali iliamua kuitoza faini ya Sh milioni 100 kwa kitendo hicho.
Alisema
zipo kampuni nyingine za ving’amuzi zinaendelea kufuatiliwa kwa ukaribu
na kuwataka Watanzania kutoa taarifa pale chaneli tano ambazo ni TBC 1,
ITV, EATV, Channel Ten, Star TV na Clouds TV zitakaposhindwa kuonekana
ili sheria ziweze kuchukuliwa haraka.
No comments:
Post a Comment