Takukuru Singida yamtia mbaroni Gulamali ( Aliyeshinda kura za Maoni CCM Jimbo la Nyalandu )
Taasisi
ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Singida
inamshikilia mshindi wa kwanza kura za maoni CCM jimbo la Singida
kaskazini, Haider Hussein Ghulamali (46), kwa tuhuma ya kutoa rushwa ya
shilingi milioni mbili taslimu kwa afisa usalama wa taifa (jina tunalo).
Lengo
la Ghulamali mfanyabiashara na mmiliki wa kiwanda cha magodoro mjini
Dodoma,ni kwamba afisa usalama huyo amtolee taarifa nzuri Kwenye vikao
vya ngazi za juu, ili aweze kuthibitishwa na vikao hivyo, kuwa mgombea
ubunge jimbo la Singida kaskazini.
Mkuu
wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Joshua Msuya, alisema Ghulamali amekamatwa
Desemba 12 mwaka huu saa 8.30 mchana, maeneo ya Rafiki resort wakati
akikabidhi rushwa hiyo iliyokuwa imehifadhiwa kwenye bahasha.
Msuya
alisema desemba 11 mwaka huu,ofisi yake ilipata taarifa ya kuwepo kwa
vitendo vya rushwa kwa mmoja wa wana CCM anayewania ubunge jimbo la
Singida, ambaye ni Ghulamali.
“Baada
ya kupokea taarifa hiyo uchunguzi ulianza ikiwa ni pamoja na kuchunguza
vitendo rushwa alivyofanya mtuhumiwa huyo, kabla na baada ya kura za
maoni kupigwa desemba 10 mwaka huu huko kijiji cha Ilongero.Kura hizo
zilimpitisha Ghulamali aliyepata kura 606 kati ya kura 1009
zilizopigwa,” alisema.
Mkuu
huyo, alisema baada ya zoezi hilo kupita la kura za maoni,mtuhumiwa kwa
juhudi zake aliweza kupata namba za simu za afisa wa usalama wa taifa
ambaye walikuwa hawafahamiani.
“Baada
kupata namba ya simu ya afisa usalama taifa, Ghulamali aliweza kumpigia
na akatoa maombi yake ya kusafishiwa taarifa kwenye vikao vya juu.Baada
ya maombi hayo,aliweza kutoa rushwa ya shilingi milioni mbili,na
kumkabidhi afisa huyo. Ndipo alipokamatwa na TAKUKURU waliokuwa wameweka
mtengo,” alisema Msuya.
Alisema
uchunguzi zaidi bado unaendelea kuhusiana na mtuhumiwa Ghulamali kabla
ya uchaguzi na baada ya uchaguzi wa kura za maoni.
Mkuu
huyo wa TAKUKURU,ametoa rai kwa wanachama wa vyama vyote vya
siasa,wagombea na wananchi kwa ujumla, kuzingatia sheria za uchaguzi
ndani ya vyama vyao.Pia kujiepusha na vitendo vya rushwa nyakati za
uchaguzi ndani vyama.
“TAKUKURU
itamkamata mgombea,mpambe na mwanachama yeyote atakayejihusisha na
vitendo ya kuomba na kupokea rushwa,na ikipata ushahidi wa
kutosha,itamfikisha mhusika mahakamani,” alisema Msuya.
No comments:
Post a Comment