Trending News>>

Serikali yatishia kuzifuta Taasisi za dini zinazokiuka misingi ya kuanzishwa kwake





Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kidini Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi chini ya Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002 (Societies Act) inazikumbusha Jumuiya zote zilizosajiliwa chini ya Sheria hii, kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria pamoja na masharti ya usajili waliopewa wakati wa usajili. Miongoni mwa masharti yanayopaswa kuzingatiwa na Jumuiya hizo ni pamoja na kutoa taarifa za mabadiliko ya Katiba zao ambazo pamoja na mambo mengine hueleza malengo ya Jumuiya husika.
Hata hivyo, baadhi ya Jumuiya zimekuwa zikifanya shughuli zao kinyume na malengo yaliyomo kwenye Katiba zao bila kuiarifu Ofisi ya Msajili. Mathalani hivi karibuni kumekuwepo na tabia ya baadhi ya viongozi wa Jumuiya kutumia mahubiri yao wakati wa ibada kuchambua masuala ya siasa kinyume na Katiba zao kwani hakuna Jumuiya yoyote iliyosajiliwa chini ya Sheria ya Jumuiya ili kufanya kazi za siasa. Tabia hii ni kwenda kinyume na malengo na ni ukiukaji Kanuni ya 7 ya Kanuni za Jumuiya zilizoundwa chini ya Sheria ya Jumuiya, inayotamka, kati ya mengine kwamba Jumuiya yoyote hairuhusiwi kufanya mabadiliko ya malengo yake bila ya kibali cha Msajili’’.
Ofisi ya Msajili inazikumbusha Jumuiya zote zinazofanya kazi kinyume na malengo yaliyoainishwa katika Katiba zao zilizosajiliwa kuacha kufanya hivyo mara moja. Aidha Ofisi ya Msajili inazikumbusha Jumuia zote kwamba ukiukaji wowote wa Sheria ni kosa ambalo linaweza kupelekea Jumuiya husika kufutiwa usajili wake kama ilivyoelezwa kwenye kifungu cha 17 cha Sheria husika.
Imetolewa na:
Meja Jenerali Projest Rwegasira (Mstaafu)
KATIBU MKUU
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

No comments:

Powered by Blogger.