Trending News>>

Rais Magufuli: "Airtel kwa taarifa tulizo nazo, ni mali ya TTCL......Pamefanyika tu michezo ya hovyo hovyo"

RAIS John Magufuli amesema Serikali imebaini kuwa kampuni ya Mawasiliano ya Bharti Airtel ni mali ya Shirika la Mawasiliani Tanzania (TTCL) na amemwagiza  Waziri wa fedha na mipango kufuatilia suala hilo haraka ili Airtel irudishwe kumilikiwa na serikali.

Rais ameyasema hayo leo Desemba 20 wakati akizungumza kwenye Ofisi za Taifa za Takwimu mjini Dodoma.

“Kampuni ya AIRTEL imethibitika kuwa ni mali ya Shirika la TTCL, lakini kuna mchezo ulifanyika, sasa sitaki kuongea sana. Nataka Waziri wa Fedha ufuatilie suala hili kabla ya mwaka huu kuisha,” amesema Magufuli.

Taarifa na ndani zinabainisha kwamba hisa za Airtel  zinatarajiwa kukabidhiwa kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na kuendesha biashara za kampuni hiyo yenye wateja wengi zaidi nchini ikiwa nyuma ya Vodacom na Tigo.

Chanzo cha mpango huo kinatajwa kuwa ni uongozi wa juu wa TTCL uliotaka Serikali kudai haki zake za uwekezaji ndani ya Airtel ambako inaimiliki kwa ubia wa asilimia 40 kwa 60 na mwekezaji.
Taarifa zinaarifu kuwa  TTCL itamiliki hisa zote za Airtel Tanzania Limited ambapo tayari TTCL imewasilisha hoja ya kutaka kufanya hivyo baada ya kubaini kwamba Serikali ilipunjwa kwenye hesabu za uwekezaji.

Hoja ya TTCL inaanzia Novemba 3, 1998 ilipoanzisha kampuni tanzu ya Cellnet ambayo ilifanya kazi mpaka Mei 7, 2001 ilipobadilishwa jina na kuitwa Celtel Tanzania huku umiliki wake ukiendelea kuwa chini ya shirika hilo kwa asilimia zote baada ya kuwekeza Dola milioni tano za Marekani (zaidi ya Sh11 bilioni sasa).

Lakini, Januari 31, 2002, Celtel ikiwa chini ya umiliki wa TTCL ilikopa kiasi cha Dola 82 milioni (zaidi ya Sh180.4 bilioni) ili kukuza mtaji wake.

Kwa kipindi hicho, TTCL iliyokuwa na thamani ya Dola 600 milioni (zaidi ya Sh1.32 trilioni) ilikuwa inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Mobile System International (MSI) ya Uholanzi. Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 65 ya hisa zote na mbia huyo asilimia 35 zilizosalia.

Agosti 5, 2005, mabadiliko yalifanywa kwenye bodi ya wakurugenzi wa Celtel kwa lengo la kuunda kampuni mbili tofauti; Celtel ikitenganishwa na TTCL. Kutokana na mabadiliko hayo, Celtel iliwekwa chini ya umiliki wa MSI ambayo Septemba 2007 iliuza hisa zake kwa Zain ambayo nayo ilikuja kuziuza kwa Bharti Airtel, Juni 8, 2010.

Imeelezwa kuwa TTCL inadai uwekezaji wake ilioufanya Celtel baadaye Airtel ambayo thamani yake imeongezeka maradufu sasa haulingani na inachokipata hivyo kutaka kusimamia biashara za kampuni hiyo ya mawasiliano.
Hoja ya madai hayo ni namna umiliki wa hisa ulivyobadilishwa baada ya Celtel kutenganishwa na TTCL ambayo ilipewa hisa chache tofauti na ilivyostahili.

Kwa sasa, Airtel Tanzania inamilikiwa na Serikali yenye asilimia 40 na Celtel Tanzania BV, kampuni tanzu ya Zain Africa BV ambayo ilinunuliwa na Bharti Airtel International, Novemba, 2010 ikiwa na asilimia 60.

Katika mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni, Serikali iliilipa Bharti Airtel Sh14.7 bilioni hivyo kuchukua asilimia 35 ya hisa ilizokuwa inamiliki na kuifanya imiliki asilimia zote za TTCL.

Sheria mpya iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge imeibadili TTCL inayohudumia asilimia 0.82 ya soko kuwa shirika la umma la mawasiliano na kulipa jukumu kubwa katika sekta ya mawasiliano nchini.

Bharti Airtel inatakiwa kuorodhesha asilimia 25 ya hisa zake katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ili kukidhi vigezo vya sheria ya posta na mawasiliano ya mwaka 2010, lakini bado haijafanya hivyo.

No comments:

Powered by Blogger.