MBWA WA POLISI AMUUMBUA JAMAA ALIYETENGEZA TUKIO FEKI LA WIZI DODOMA
Mfanyakazi wa kampuni ya saruji ya Simba Cement, Edward Ngassa
amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kwa tuhuma za kutengeneza
tukio la uongo la kuporwa Sh. milioni 20.4 na majambazi jana.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, mbwa wa
polisi mwenye mafunzo ndiye aliyegundua udanganyifu huo wa Ngassa
nyumbani kwake.
Kamanda Muroto alisema mtuhumiwa huyo alitengeneza tukio la uongo kwamba
ameporwa fedha na majambazi katika eneo la Uhindini karibu na mgahawa
wa Sunja.
Kufuatia ripoti ya tukio hilo, Muroto alisema, timu ya upelelezi
ilifanya uchunguzi wa kina na kubaini kwamba hakukuwa na tukio la
uporaji katika eneo hilo.
“Katika uchunguzi huo tulienda kumpekua kwa kina mtuhumiwa nyumbani
kwake na kufanikiwa kukamata fedha zote alizoiba akiwa ameficha kwenye
ndoo ndogo ya plastiki na kuweka udongo kisha kupanda ua juu yake ili
zisikamatwe kirahisi,” alisema.
Muroto alibainisha kuwa waliweza kuzifichua fedha hizo kwa kutumia mbwa
ambaye alikuwa akinusa kwenye maeneo yote na kuzikuta kwenye ndoo ya ua.
“Huyu mtuhumiwa alimpigia simu mwajiri wake akidai kuwa wakati anaelekea
benki kuna pikipiki ya majambazi ilimzuia kwa mbele na kumpora hizo
fedha,” alisema Muroto.
Katika hatua nyingine, Kamanda Muroto alisema watu wawili wamekamatwa
kwa wizi wa betri tatu za minara ya mawasiliano katika eneo la
Chang’ombe na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
“Watuhumiwa Eliezel Muhongole ambaye ni fundi na mfanyakazi wa kampuni
ya Halotel na Alfredy Mlugu mkulima na mkazi wa Mpunguzi walikamatwa kwa
wizi huu,” alisema Muroto.
Mbali na hilo, Muroto alisema watu watatu wanashikiliwa na polisi mkoani
humu kwa kukamatwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye uzito wa
kilo 16 na thamani ya Sh. milioni 33.2.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni mkazi wa Dar es salaam Hussein Henry
(40), na Mussa Ramadhani (35) na Abdalah Ramadhani (32) wote wakazi wa
Kondoa.
“Hawa walikamatwa wakiwa wamepakia meno haya ya tembo kwenye pikipiki
yenye namba za usajili MC516 BDC aina Fekon wakitokea Kondoa wakielekea
Dodoma mjini,” alisema.
No comments:
Post a Comment