Trending News>>

Mbaroni kwa kujifanya Daktari

Jeshi la polisi mkoani Mwanza linamshikilia mtu mmoja kwa kosa la kujifanya daktari, katika hospitali ya mkoa Sekou Toure.

Joseph Mbagata 25,mkazi wa mtaa wa Mabatini jijini humo amekamatwa leo Desemba 18  na jeshi hilo baada ya kubainika kwamba sio mwanataaluma na alikuwa akiwatapeli wagonjwa kwa kuwaomba hongo, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Taarifa kutoka kwa jeshi hilo zimesema kwamba mtuhumiwa alikuwa akiwaomba hongo, huku akiahidi kuleta dawa muhimu na pia kufanya mipango ili mgonjwa apate huduma kwa haraka.

Awali zilipatikana taarifa kuwa siku chache zilizopita alionekana mtu aliyevalia mavazi ya udaktari na kujifanya daktari, kisha anapita wodini kuwaona wagonjwa. Pia ilisemekana kuwa mtu huyo tayari amechukua Sh30,000  kwa mgonjwa ili aweze kumpatia matibabu.

Aidha baada ya tuhuma hizo kufika katika uongozi wa hospitali waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa, akiwa amevalia mavazi ya udaktari huku akiwa amesimama nje ya wodi ya upasuaji.

“Tumekuwa tukilalamikiwa kwamba kuna baadhi ya madaktari hapa hawana ujuzi wala hawajitambui, kumbe ni dhahiri kwamba hao watu wapo na kuanzia sasa lazima tufanye ukaguzi wa hali ya juu ili hali hiyo isije ikajitokeza tena maana ni sehemu ya kuhatarisha maisha,” amesema  mmoja wa madakatri katika hospitali hiyo ambaye hakutaka kutajwa majina.

Baada ya daktari huyo feki kukamatwa, uongozi wa hospitali ulitoa taarifa polisi, ambapo askari walifika eneo la tukio na kumuweka mtuhumiwa chini ya ulinzi kisha kumfanyia upekuzi kwenye begi alilobeba na kukuta mavazi yanayotumiwa na madaktari katika vyumba vya upasuaji.

Polisi wapo katika upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza naibu kamishina wa polisi Ahmed Msangi ametoa wito kwa wananchi hususani wagonjwa waliopo hospitalini akiwaomba kuwa makini na watu ambao ni matapeli wa aina kama hiyo wenye nia ovu dhidi yao.

Aidha pia aliwaomba viongozi wa hospitali zote kuendelea kutoa taarifa kwa polisi kuhusiana na watu wanao watilia shaka hospitalini, ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Mwananchi.

No comments:

Powered by Blogger.