Mabinti Wanaswa Wizi wa Pikipiki, Sare za Jeshi
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam limewakamata watu watatu, wakiwemo mabinti wawili wa miaka 19,
kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa pikipiki jijini humo.
Hayo yamesemwa leo na Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa wakati akizungumza na
wanahabari jijini Dar alipokuwa akitoa taarifa ya oparesheni maalum
katika kukabiliana na uhalifu.
“Tumekamata watu watatu kwa tuhuma za
wizi wa pikipiki lakini miongoni mwao ni mabinti wawili wa miaka 19
ambao wanatuhumiwa kutumika kama chambo ili kufanikisha mazoezi ya wizi
na matukio mengine ya uhalifu.
“Pia tumefanikiwa kuwakamata watu
wawili wanaodaiwa kuiba sare za jeshi, ambapo wanatuhumiwa kutumia sare
hizo kufanya wizi na matukio mbalimbali ya uhalifu,” alisema Mambosasa.
Aidha jeshi hilo litawafikisha mahakamani watuhumiwa hao pindi litakapokamilisha uchunguzi wake.
Akizungumzia kuhusu Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, Kamanda Mambosasa amesema:
“Kuelekea msimu huu wa Sikukuu,
tumejipanga vizuri kufanya doria, mpaka sasa jiji la Dar liko salama.
Niwaonye wahalifu msijidanganye kujaribu kufanya mabo ya ajabu, tuko
imara kuhakikisha Sikukuu zinamalizika salama.”
Mambosasa amepiga marufuku ‘disko
toto’ kwa kuwa disko hizo nyingi hazijakidhi vigezo. Pia amewataka
wazazi kufuata njia salama ya kuwafurahisha watoto wao katika siku hiyo
ya Sikukuu.
“Tumeamua eneo la Tanganyika Packers,
Kawe, kuwa ni eneo maalum la kusheherekea kipekee Siku ya Mwaka Mpya.
Pia ni marufuku mtu kufyatua fataki siku ya Mwaka Mpya. Tutatoa nusu saa
tu katika eneo la Tanganyika Packers kuwa sehemu maalum ya kupiga hizo
fataki,” alieleza Mambosasa.
No comments:
Post a Comment