ABIRIA WAONYWA KULA HOVYO WAKIWA SAFARINI MSIMU HUU WA SIKUKUU.
Abiria wanaosafiri katika msimu huu wa kuelekea sikukuu
wametahadharishwa kutokula au kunywa vitu watakavyopatiwa ndani ya
magari na watu wasiowafahamu.
Pia wametakiwa kutoa taarifa kwa wakati pindi watakapoona kuna
ukiukwaji wa sheria na kanuni za usafirishaji ikiwa ni pamoja na kutozwa
nauli tofauti na iliyopangwa pamoja na mwendo kasi au mtu yeyote
atakapofanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wao.
Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa Desemba 15 wakati Mamlaka ya Usafiri wa
Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi
mkoani Mtwara wakifanya operesheni katika mabasi ya abiria kituo kikuu
cha Mtwara kabla ya kuanza safari ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa
madereva, kondakta pamoja na abiria.
Akizungumza na abiria mkaguzi wa magari wa kikosi cha usalama
barabarani, Said Masoud amewatahadharisha abiria kutokula hovyo vitu
watakavyopatiwa kwenye magari na watu wasiowafahamu.
“Tunaelekea kipindi cha Krismasi na mwaka mpya ni kipindi cha hatari
sana watu wako kazini, usimwamini uliyekaa naye kama humfahamu mmekutana
kwenye kiti anakupa pipi unakula, anakupa karanga unakula utaumia
nawatahadharisha tena watu wapo kazini mmekutana kwenye gari salimianeni
kama abiria ila usimuhisi kwamba hiyu ndio mwizi ili mkae kwa amani
mfike salama,” amesema Said.
No comments:
Post a Comment