Unatamani Ndoa? Uko Tayari Kwa Mishare?
UNAPOONA bibi harusi yupo ndani ya shela, bwana harusi amepiga suti kali huwa inapendeza, unaweza kuona mambo ni rahisi tu.
Wengi wanapowaona maharusi, huwa nao wanaitamani. Mtu anatamani na
yeye siku moja aingie. Mwanamke anavutiwa na shela, mwanaume anavutiwa
na suti.
Kila mmoja anaguswa kwa upande wake. Kuna ambao wanavutiwa na jinsi
watu wanavyowaheshimu maharusi, wanavyowapa ule ‘uspesho’ wa ndoa.
Wao ndio siku yao, wanakusanya umati wa watu wa pande zote mbili, ndugu jamaa na marafiki kuja kushuhudia tukio hilo takatifu.
Wazazi wa pande zote mbili wanafurahi. Wazazi wa bwana harusi
wanafurahi mtoto wao amepata jiko. Wazazi wa upande wa bibi harusi
wanasherehekea zaidi kwa binti yao kuwapa heshima ya kuingia kwenye
daraja la ndoa.
Wanamshukuru Mungu maana si wote wanaopata bahati hiyo. Wengi huishia
kuzalishwa, ndoa wanazisikia kwa jirani. Umri unawatupa mkono,
wanapoteza dira na mwelekeo na kukata kabisa tamaa ya ndoa.
Bahati mbaya sana uhusiano wa kimapenzi unawahusisha watu wawili.
Wapendanao ndio wanaojua safari yao ikoje. Wengi huwa wanafikiri labda
watu huibuka tu kama uyoga na kujikuta wameingia kwenye ndoa.
Nimekuwa nikifundisha mara kadhaa katika makala zangu. Penzi la kweli
huwa lina historia. Safari ya uhusiano ina milima au mabonde. Ina shida
na raha. Si rahisi sana ukiwaona watu wamependeza, wameshikana mikono
kama mke na mume kuwafikiria kwamba wamepitia shida nyingi.
Kuishi na mtu ambaye mmekutana ukubwani kunahitaji ‘rehema’ za Mungu. Kunahitaji
uvumilivu. Kunahitaji maelewano yatakayowafanya wapendanao wazungumze
lugha moja. Tofauti na hapo watu hujikuta kwenye sarakasi za kila
uchwao.
Hiyo ndiyo ninayoita mishale. Ukipata bahati ya kuzungumza na
wanandoa wengi unaowajua, watakuambia ni Mungu tu. Hawaamini kwamba kwa
mapito yao yalivyokuwa magumu kama wangeweza kufanikisha safari yao
wakiwa pamoja.
Wengi wana historia ya mambo makubwa ya kukatisha tamaa. Wapo walio
kosanakosana na mapanga katika safari yao. Wapo waliofumaniana. Wapo
ambao watakuambia walishagombana vya kutosha hadi kufikia hatua ya
kuachana kisha baadaye kurudiana.
Hakuna ‘kirusi’ kibaya na kinachouma kama usaliti. Wapo ambao katika
historia ya uhusiano wao, utakuta mara kadhaa wameshakumbana na kisanga
hicho. Wamefanikiwa kukivuka. Wapo wanawake waliowavumilia wanaume zao
walevi kiasi cha kuvuka mipaka.
Wapo wanaume waliowavumilia wanawake wao walevi kupita maelezo.
Mwisho wa siku waliamua kuchukuliana. Kukubaliana na changamoto kisha
kusonga mbele.
Ndio maana mara nyingi hutokea kwenye harusi, watu wanashuhudia bibi harusi akilia sana hadi watu kuhoji kulikoni.
Analia kwa uchungu na furaha. Anakuwa haamini kilichotokea,
akirudisha kumbukumbu nyuma juu ya safari yao, machozi lazima
yabugujike. Anayaona magumu waliyoyapitia. Wengi wameshindwa kuyabeba na
kujikuta wakikatisha safari zao mapema.
Uvumilivu katika uhusiano ni suala la msingi. Usiwe mwepesi wa kukata
tamaa. Usitamani tu ndoa ukafikiri maisha ya ndoa ni mepesi. Yana
shuruba zake. Yanahitaji kuchukuliana tabia. Yanahitaji kusikilizana,
kurekebishana kwa staha pale mnapoona kuna tatizo.
Yanahitaji kujishusha. Kunapotokea mtafaruku, mmoja wenu akishuka,
hakutatokea shari. Ukiona mwenzako amepaniki kwa kitu fulani, ni jukumu
lako kushuka na kumrudisha katika hali ya kawaida. Ni kosa kubwa kupanda
juu wakati mwenzako naye amepanda.
Kuna majungu, kuna maneno ya kizushi lazima kila mmoja awe na busara
na hekima katika kushughulikia mambo yanayoibuka katika safari yenu.
Usiambiwe tu mwenzako kakusaliti na wewe ukalibeba kama lilivyo na
kuanzisha vurugu.
Jipe muda kidogo, chunguza na ukiona kuna ukweli tafuta njia ya
kukabilana na tatizo husika. Usipaniki katika kushughulikia suala hilo
kwani unaweza kujikuta umeharibu kwa mtu ambaye pengine ni mtu sahihi
maishani.
#MANYAMAJR
No comments:
Post a Comment