Penzi Bora Linajengwa Na Imani, Ishughulikie!
KWA mapenzi ya Mungu, tunakutana hapa kwa mara nyingine tena. Kwa ajili ya kupeana darasa la uhusiano. Kwa hakika, kupitia ujumbe mnaonitumia, ninaamini mnajifunza mambo mengi na mtaendelea kubadilika. Kwa kuwa kila mmoja wetu anahitaji kudumu kwenye uhusiano wake, ni vyema kuzingatia yale ambayo mara kwa mara nimekuwa nikiyaandika kwenye safu hii. Mapenzi yana pande mbili, mwanaume na mwanamke. Kila mmoja ana hulka, mila na desturi zake, hivyo ili muweze kudumu lazima mshabihiane kitabia.
Kila mmoja awe tayari kubadilika pale anapoona amekengeuka. Kwa kawaida binadamu tulivyoumbwa, mara nyingi kila mmoja wetu anajiamini yeye kwanza. Anaamini yupo sawa. Kila anachokifanya yeye kinakuwa ni sawa, hakosei. Akitokea mtu wa kumsahihisha, anamuona yeye ndiyo mkosaji. Panapotokea kila mmoja akajiona yupo sahihi, hapo ndipo panapotokea mtafaruku. Penzi linageuka chungu. Wapendanao wanagombana. Wanavutana na mwisho wa siku wakishindwa kuelewana, wanaishia kuachana.
Nikirudi katika mada ya leo, inahusu imani. Marafiki zangu, imani ndiyo kila kitu. Suala la imani inajengwa na mtu mwenyewe. Linapokuja suala la uhusiano, unapotanguliza kutokuwa na imani utapata shida. Jambo la kwanza na la muhimu unalopaswa kuwa nalo ni imani. Kama umeshamchunguza mpenzi wako, ukajiridhisha ana sifa za kuwa mpenzi, mchumba na baadaye mke au mume, huna budi kumuamini. Hakikisha umejiridhisha katika hatua za awali kabla ya kuzama penzini, jiulize mtu uliyenaye anafaa? Ana sifa za kuwa mume au mkeo?
Usije kupita hatua hizo za awali bila kujiridhisha maana huko mbeleni utatengeneza bomu ambalo likija kulipuka litakuwa na madhara makubwa. Mchunguze ana mapenzi ya dhati? Ana utu? Ni mvumilivu? Ana malengo ya muda mrefu au mfupi? Ana hofu ya Mungu? Ana tabia njema? Ukijiridhisha hayo yote ndipo uingie kwenye hatua kubwa na ya muhimu niliyoizungumzia hapo juu, imani. Muamini kweli kweli.
Kuwa na imani kwamba uliyenaye anakupenda kwa dhati, anakuheshimu na anakujali. Weka imani kwamba kamwe hatoweza kukusaliti. Mjengee mazingira ya kwamba hata ikitokea amekusaliti, nafsi imsute. Ajione kweli ni mkosaji na hakustahili kukufanyia hivyo kwani wewe mpenzi wake ni mwaminifu na unamuamini. Aone kabisa kitendo chake cha kukusaliti ni kukupa wewe maumivu ambayo hustahili.
Aumie maana
akitafakari kwamba wewe husaliti halafu yeye amesaili, kwa binadamu anayejua kujifanyia tathimini hakika atabaini kwamba amekukosea. Anaweza asikuombe radhi lakini moyoni anajutia uamuzi wake. Wanawake, ngoja niwamegee siri. Mara nyingi wanaume hujikuta wakijilaumu. Mwanaume anapomtafakari mwanamke wake, kwamba ni mvumilivu, mstarabu, mnyenyekevu na muaminifu anajisikia
vibaya pale anapomtendea jambo baya. Anahisi anamtenda asivyostahili.
Anaweza asiombe radhi lakini mara nyingi wanaume wanaokutana na hali hii hujikuta wakitafuta hata zawadi na kuwapa wanawake zao. Mwanamke huna hili wala hili, anashangaa paap, kitenge! Hataki kukiri kwamba amekosea lakini moyoni anajuta. Huwezi kumchunga mpenzi wako kama mbuzi, jenga desturi ya kumuamini. Jenga imani
kwamba hatakusaliti na kweli hatakusaliti. Ukiwa kila wakati unasalitiwa, kweli unaweza kusalitiwa. Yawezekana akawa hakusaliti lakini kwa kutoonesha imani kwake, anaweza kukereka na vitendo vyako.
Kuwa na shaka naye kila mara, kumuuliza upo wapi unafanya nini au kwa nini unachelewa kurudi wakati nwingine vinaweza kumnyima amani mwenzi wako na matokeo yake mkaanza kugombana. Imani inakuweka huru, muamini kwanza hayo mengine muachie Mungu. Muombe amuongoze mwenzi wako awe na hekima, awe na busara, asipate tamaa ya kukusaliti. Ukijijengea imani utaishi vizuri na hata kama itatokea mwenzi wako amekusaliti na umegundua, utatumia hekima kuzungumza naye, kama kweli anakupenda, atatubu na mtaendelea na safari yenu.
No comments:
Post a Comment