Makamu wa Rais – Tumieni malighafi zenu kwa viwanda vya ndani ya nchi zenu
Serikali imezitaka nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki
kutumia malighafi zinazopatikana katika nchi hizo kwa ajili ya viwanda
badala ya kuagiza kutoka nje.
Rai hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua
Mkutano wa Pili wa Biashara na Ujasiriamali ya Afrika Mashariki.
“Ndoto yetu ya uchumi wa viwanda sio kuhamishia viwanda
vya nje hapa nchini bali ni kuwa wabunifu na kujenga viwanda vyetu
wenyewe,”amesema Samia.
Amesema ujenzi wa uchumi wa viwanda uendane na kufanya kilimo chenye tija ambacho kinalenga kuwaondolea umaskini wananchi.
“Wakulima wetu hawana uhakika na soko la mazao yao kwani
wanapopata mazao kwa wingi, bei inashuka, wakati wa ukame mazao
yanaharibika, hivyo kwao nyakati zote ni taabu,” amesema Mhe. Samia.
Makamu wa Rais amewataka wakulima waongeze thamani ya mazao yao
badala ya kuuza mazao ghafi. Kwa kufanya hivyo watajiongezea kipato na
kuondokana na umaskini.
Uanzishwaji wa viwanda katika Jumuiya ya Afrika mashariki utasaidia
katika kuinua kilimo kwani mazao hayo yatapata uhakika wa soka kwenye
viwanda hivyo.
Amezitaka nchi hizo kutengeneza ajira hasa kwa vijana ambao takwimu
zinaonyesha kuwa ndio wengi, hivyo ni muhimu kuwapa kipaumbele.
Serikali na sekta binafsi zimetakiwa kufanya juhudi za makusudi
kuanzisha viwanda ambavyo vitaongeza ajira na kuifanya Tanzania kuwa na
uchumi wa viwanda.
Aidha, Mhe. Samia amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
kudumisha amani kwani bila amani uwekezaji katika viwanda na maeneo
mengine hauwezekeni.
Amani ni bidhaa adimu ambayo inapatikana kwa gharama, hivyo siyo ya kuchezea bali ni ya kulindwa, aliongeza Mhe. Samia.
Huu ni Mkutano wa Pili ambao unajumuisha washiriki kutoka, Kenya,
Burundi, Rwanda, Uganda na wenyeji Tanzania. Katika Mkutano huo
yanafanyika maonyesho ya wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashiriki.
Imetolewa na MAELEZO
No comments:
Post a Comment