Trending News>>

Mwanaume Uwe Bosi Kwa Mwanamke Unaachaje Kuwa?

KUTOKANA na ubize wa maisha, wanaume wengi sana wamekuwa wakishindwa kutimiza majukumu yao. Mwanaume anashindwa kufanya mambo yanayompasa kufanya kwa mwenzi wake na kujikuta akiingia kwenye migogoro na mwenzi wake. Ubize huu upo wa aina nyingi.

Kuna ambao majukumu ya kazi yanawabana wanajisahau lakini kuna ambao wanafanya makusudi kwa kubebwa na zile kauli za ‘atanifanya nini mimi si ndiyo mwanaume.’ WANAKOSEA Mapenzi yana vikorombwezo vingi ili yaweze kuwa na tija. Mwanaume anapaswa kumpa ulinzi mwanamke ili aweze kujivunia kuwa na mwanaume wake.

Anataka atambe kuwa na mwanaume ambaye ndiyo shujaa wake. Ukimtimizia mahitaji yake, atajiona wa thamani na atakuheshimu zaidi. Mwanaume unapaswa kumpa ulinzi wa kutosha mwanamke wako kwa kuhakikisha unampa mahitaji yote anayoyahitaji. Mwanaume unapaswa kuwa bosi wa mkeo. Kwa kawaida mwanaume ni kichwa cha familia.

Hilo liko wazi na halihitaji mjadala. Usiwe kichwa katika kutoa amri za kufuliwa nguo, kuwekewa chakula na mambo mengine lakini ukasahau suala zima la kuwa mwezeshaji. Mwanaume unapaswa kuwa mwezeshaji ili kweli uweze kuibeba dhana ya ‘kichwa.’ Unaanzaje kubebwa tu maisha yako yote na mwanamke?

Dunia itakushangaa! Hata kama inatokea mwanamke anakuzidi kipato, usibweteke. Lazima uanaume wako uonekane katika maisha ya kila siku. Usiwe mzigo. Fanya kazi kwa bidii. Usiwe mwanaume suruali kama wanavyosema vijana wa siku hizi.

Mwanamke naye asikubali. Amuinue mwanaume wake ili aweze kuwa kichwa. Mwanaume hakikisha unafanya jitihada za makusudi uweze kujitanua kipato chako hata kwa kupitia huyo mwenzi wako lakini mwisho wa siku, kibusara, mwanaume uwe ‘mtawala’. Siyasemi haya kwa maana ya kuwa nasisitiza mfumo dume, la hasha. Nasema haya kwa maana ya kuwainua wanaume wote watambue kwamba wana wajibu wa kutafuta mahitaji kwa ajili ya mke pamoja na familia yake.

Mwanaume anapaswa kuakisi maagizo ya kutafuta kwa jasho yaliyoandikwa hata katika vitabu vya dini: “Kwa kuwa wewe umemsikiliza mkeo, ukala matunda ya mti ambayo nilikuamuru usile; kwa hiyo kwa kosa lako ardhi imelaaniwa. Kwa jasho utajipatia humo riziki yako siku zote za maisha yako.” Mwanzo 3:17. Hayo yalikuwa ni matokeo ya adhabu ambayo Mungu aliitoa kwa Adam baada ya kuingia mkenge wa Eva.

Usisahau Eva naye alipewa adhabu yake baada ya kuukubali mkenge wa nyoka. Hivyo ndivyo ilivyokuwa, na hii hata uwe huna dini, hakika utaungana na mimi kwamba mwanaume ana majukumu yake, mwanamke anayo yake kiasili. Mwanaume alitangulia, mwanamke akaumbwa kutokana na mwanaume, jifunze hii: “Amewaumbieni wake zenu kutokana na nyinyi.’ (Suratul Nisaa, Suratul Aali Imran na Suratul Ruum).

Mwanaume atimize majukumu yake. Nani atakucheka akisikia unaihudumia familia? Nani atakushangaa akisikia ndiyo unayemgharamia mkeo saluni, mavazi na mahitaji yake madogomadogo? Mtu atamshangaa mwanaume kama akiwa anamtegemea mwanamke. Atakucheka ukiwa unalelewa. Utaonekana wa ajabu pia kwani unaenda kinyume na mpango wa Mungu. Raha ya mwanaume ni kupambana. Kuwa chanzo cha mapato. Kumgharamia mwenzi wako. Atajisikia ufahari endapo utamgharamia mahitaji. Atajiona wa thamani mbele ya wenzake. Atajua unampenda, unamjali. MJALI SANA Wanaume wengi wanajisahau sana. Wenzi wao wanawajali kwa hali na mali lakini wao hawarejeshi sawasawa na wenzi wao. Mjali, mthamini kwa mambo madogomadogo ambayo yanachochea upendo.

No comments:

Powered by Blogger.