Trending News>>

Kataa Kudharaulika, Zingatia Haya Jamii Ikuheshimu!!!!!!

Kataa Kudharaulika, Zingatia Haya Jamii Ikuheshimu!


NINA kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa mema ambayo amekuwa akinitendea katika kila siku ya maisha yangu. Kikubwa nimshukuru kwa kunijaalia uzima kiasi cha kuniwezesha kuendelea kuwa hai na kukutana nanyi tena kupitia ukurasa huu.
Wiki hii nitazungumzia juu mambo mbalimbali ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kukufanya usidharaulike bali watu wanaokuzunguka wakuheshimu na kukuchukulia kama mtu muhimu.
Kila mtu anapenda kuheshimiwa, sidhani kama yupo mtu ambaye anafurahi kudharaulika na kuonekana asiye na manufaa kwa jamii yake.
Hiyo ndiyo imewafanya baadhi ya watu kufanya kadiri wawezavyo, kwa gharama yoyote kuhakikisha kwamba wanapata heshima ambayo wanastahili kuipata mbele ya jamii.
Wapo baadhi ya watu wanaoamini kwamba heshima kwa binadamu hupatikana kwa kuwa na umri mkubwa, uwezo kifedha, elimu, sehemu anayoishi na vigezo vingine vya namna hiyo. Hiyo sio kweli licha ya kwamba vitu hivyo kwa upande mwingine vinaweza kumfanya mtu akaheshimika.
Elewa kwamba unaweza kuwa na umri mkubwa, fedha nyingi, elimu ya juu lakini bado ukawa unadharaulika. Wanasaikolojia wanaeleza kwamba, heshima haiwezi kupatikana kwa njia ya mkato bali hupatikana kwa kuweka misingi imara ya muda mrefu.
Ni vugumu sana kujijengea heshima kwa siku moja, wiki ama mwezi mmoja ila ninachotaka kukusisitiza ni kutumia gharama yoyote kuhakikisha unajijengea mazingira ya kuheshimika katika jamii unayoishi. Unapokuwa na heshima hakikisha unailinda heshima yako.
Wapo watu ambao huwa hawajali kupoteza heshima yao waliojijengea kwa muda mrefu badala yake huanza kufanya mambo ya aibu katika jamii kiasi cha kuweza kuipoteza heshima yao. Kumbuka unaweza kujijengea heshima kwa miaka mingi lakini ikaja kupotea kwa siku moja tu.
Kuwa makini sana na kwa kwa kukusaidia leo nitatilia mkazo katika mambo ambayo unatakiwa kuyazingatia katika kukufanya uonekane ni mwenye thamani na uheshimike.
UPENDO KWA WOTE
Yawezekana Mungu akawa amekujaalia kuwa na mafanikio makubwa katika maisha yako. Mafanikio hayo yasikubadilishe kitabia. Wapende watu wote bila kujali jinsia, kipato wala kabila. Kwa kufanya hivyo utajijengea heshima na kupendwa na kila mtu.
SAIDIA INAPOBIDI
Kuwa mtu wa kusaidia pale ambapo utatakiwa kufanya hivyo. Ninapozungumzia msaada simaanishi msaada wa kifedha tu. Unaweza kutoa hata msaada wa ushauri. Kama Mungu amekubariki kuwa na uwezo kifedha wasaidie wale wasiojiweza kwani kwa kufanya hivyo faida yake ni kubwa ukiachilia hiyo ya kupata heshima kutoka kwa watu wanaokuzunguka.
MANENO YAKO
Jinsi unavyozungumza mbele ya watu pia kunaweza kukusaidia katika kukujengea heshima katika jamii. Kusema ovyo na kutamka maneno machafu mbele ya watu huweza kukupunguzia heshima yako. Tambua kwamba, jinsi unavyozungumza inaweza kuwa rahisi kwa mtu kukutafsiri kuwa wewe ni mtu unayestahili kuheshimiwa ama kudharauliwa. Unatakiwa kuwa makini sana katika kila neno unalolitamka. Ukijaribu kuchunguza utakuta wengi waliojijengea heshima katika jamii si waongeaji sana na hata wanapoongea huwa makini sana.
TABIA ZAKO
Kimsingi zipo tabia ambazo ukiwa nazo ni vigumu sana watu kukuheshimu hata kama utakuwa mtu mzima ama una fedha nyingi kiasi gani. Miongoni mwa tabia ambazo zinaweza kukufanya usiheshimike ni kujiona, kiburi, dharua na majivuno.
Tabia hizo hutakiwi kuwa nazo kama kweli unataka uheshimike katika jamii. Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unakuwa na tabia ambazo kila mtu atakupenda na kukupa heshima unayostahili. Kama wewe ni msomi, jitahidi sana kujiepusha na tabia ya dharau dhidi ya wale wasio na elimu kama yako kwa kuona kwamba hawawezi kukusaidia kwa lolote. Unapaswa kushirikiana nao katika kila jambo ndipo watakuheshimu na kukupenda.
MUONEKANO WAKO
Heshima siku zote huanzia kwenye vitu vidogo ambavyo wakati mwingine unaweza kuvidharau lakini vina nafasi kubwa sana katika kukupa heshima mbele za watu. Mojawapo ni mavazi usafi wa mwili. Ni ukweli ulio wazi kwamba mavazi yanaweza kumshushia ama kumuongezea mtu heshima mbele ya watu. Kwa mfano, Mbunge wa jimbo fulani anapoamua kuvaa suruali pana inayoshuka mpaka kenye makalio kama wafanyavyo vijana wa siku hizi, ni wazi atakuwa amejishushia hadhi mbele ya jamii.
Au mwalimu anapovaa kimini na ‘kitop’ kilichoacha wazi sehemu kubwa ya mwili wake, ni lazima wanafunzi, wazazi, walimu wenzake na jamii kwa ujumla watashindwa kumheshimu.Hawawezi kumheshimu kwa sababu yeye mwenyewe ameshindwa kujiheshimu. Nimalizie kwa kusema kwamba, kama unataka uheshimike, anza kujiheshimu mwenyewe ndipo wengine watakuheshimu. Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.

No comments:

Powered by Blogger.