Trending News>>

Wadukuzi 10 hatari zaidi wa kompyuta duniani!


Wadukuzi wanatumia maarifa yao ya kipekee kufikia au kupata taarifa nyeti kwa njia isiyo halali. Kutumia maarifa siyo kitu kibaya au kisicho halali, bali tatizo linaanza pale ambapo maarifa hayo yanatumika kuvunja sheria.

Wadukuzi hutafuta madhaifu kwenye mifumo mbalimbali ya kompyuta na kisha kuyatumia kuiba taarifa au kufanya uhalifu mwingine.

Kutokana na kukua kwa ulimwengu wa teknolojia ya intaneti, idadi ya wadukuzi imeongezeka sana. Wadukuzi mbalimbali wamekuwa wakiishangaza dunia kwa jinsi wanavyotumia maarifa yao ya kipekee kufanya matendo ambayo ni tishio.

Naamini ungependa kufahamu baadhi ya wadukuzi waliotisha zaidi duniani. Fuatilia makala hii nikujuze wadukuzi 10 hatari zaidi wa kompyuta.

1. Gary McKinnon
Mnammo mwaka 2001, McKinnon mzaliwa wa Scotland alitumia maarifa yake ya msimamizi wa mfumo (system administration) wa kompyuta kuingilia mfumo wa kompyuta wa jeshi la Marekani. Alipoingilia mfumo huu alifuta mafaili muhimu na kupelekea hasara ya maelfu ya dola. Mdukuzi huyu alituhumiwa kwa kutekeleza udukuzi mkubwa kwa jeshi ambao haujawahi kutokea.

2. Michael Bevan na Richard Pryce
Wadukuzi hawa kwa pamoja waliingilia kompyuta za jeshi la anga la Marekani, NASA, na NATO mnamo mwaka 1996 na kuhamisha na kufuta mafaili kadhaa. Tukio hili lilikaribia kusababisha vita kati ya Marekani na Korea kaskazini kutokana na kuvuja kwa taarifa za siri juu ya mpango wa nyuklia kwenye jeshi la anga la Marekani (USAF).

3. Kevin Mitnick
Mitnick anafahamika kwa kuingilia mifumo ya simu na makampuni ya kompyuta pamoja na kubadili taarifa muhimu kwenye seva husika za kompyuta. Alikuwa akijihusika pia kuiba nywila (password) ili kuingia kwenye barua pepe kadha wa kadha. Mitnick alikamatwa mwaka 1995 na kushitakiwa kwenda jela miaka mitano. Jambo la kushangaza sasa Mitnick  anaendesha kampuni ya kuwasaidia watu kujilinda na wadukuzi kwenye mtandao.

4. Vladimir Levin
Kwa kutumia maarifa yake ya udukuzi, Levin ambaye ni raia wa Urusi aliingia kwenye seva za benki ya Citibank na kuiba dola milioni 10 kutoka kwenye akaunti mbalimbali. Baadaye alikamatwa huko Uingereza, lakini Citibank waliweza kupata dola 400,000 tu kati ya milioni 10 zilizoibiwa.

5. Michael Calce
Calce alifahamika kwa jina la MafiaBoy. Akiwa mwanafunzi wa sekondari huko Quebec Canada, Calce alitekeleza aina ya udukuzi unaojulikana kama DDoS attack kwenye tovuti maarufu kama vile Yahoo, FIFA, Dell, Amazon, eBay na CNN. DDoS attack ni udukuzi ambao wadukuzi huzalisha maelfu au hata mamilioni ya watumiaji bandia wanaotoka kufikia tovuti fulani kwa wakati mmoja; kwa kufanya hivi tovuti husika huzidiwa kwa kushindwa kuwamudu na kuisababisha isipatikane.

Waathiriwa wa udukuzi huu wa Calce walishangaa jinsi udukuzi ulivyokuwa mkubwa, inakadiriwa kuwa udukuzi huu ulisababisha hasara zaidi ya dola bilioni moja duniani kote.

6. Jeanson James Ancheta
Ancheta aliweza kutengeneza mashine 500,000 za kutengenezea botnets; Botnets ni marobot ambayo hutumiwa kufanya DDoS attack. Hata hivyo vyombo vya dola ikiwemo FBI vilimkamata na kumshitaki kama injinia mdukuzi anayetisha.

7. Adrian Lamo

Adrian Lamo alikuwa mdukuzi tofauti na wengine kwani yeye hakuwa na makazi maalumu. Alitumia maeneo ya uma yenye mtandao kama vile intaneti cafe, migahawa n.k ili kufanya udukuzi wake. Kwa njia hii ilikuwa ni vigumu kumkamata. Lamo pia alikuwa maarufu kwa kuwaonyesha wadukuzi wengine madhaifu mbalimbali kwenye mifumo ya kompyuta. Hata hivyo baadaye Lamo alikamatwa kutokana na kuhusishwa na Wikileaks.

8. Owen Walker

Walker alitumia jina la bandia la AKILL kutekeleza uvamizi kwenye tovuti na mifumo kadha wa kadha ya kompyuta. Mdukuzi huyu anafahamika sana kutokana na kirusi chake cha Akbot, ambacho kiliingia kwenye mifumo mbalimbali ya kompyuta na kusababisha uvamizi usioisha. Inakadiriwa kuwa Akbot imesababisha hasara ya zaidi ya dola milioni 26.

9. Albert Gonzalez

Huyu ni mdukuzi wa Cuba anaedaiwa kuwa na uwezo wa kutisha sana wa kuiba kwenye kadi za kibenki na mifumo ya mashine za kutolea pesa (ATM) kwenye miaka ya 2000. Albert alitumia taarifa za wateja kwa njia isiyo halali kufanya miamala yenye thamani ya dola milioni 200 za kimarekani.

10. Astra
ASTRA ni kundi la wadukuzi linalofanya kazi hadi hii leo na bado halijabainika. Mamlaka mbalimbali zimekuwa zikilifuatilia kundi hili lakini bado hawajaweza kubainisha hasa ni wapi liliko. Wengine wadai liko China huku mamlaka za Ugiriki zikidai kuwa si kundi bali ni mwanamahesabu mwenye miaka 58 kutoka Ugiriki.

Astra inakadiriwa kuwa imesababisha hasara za zaidi ya dola za kimarekani milioni 360. Udukuzi maarufu wa kundi hili ni pamoja na kuiba mipango mbalimbali ya jeshi la Ufaransa ya silaha na ndege na kuiuza kwa watu wengine.

Naamini sasa utafikiri tofauti kuhusu maswala ya usalama wa kompyuta. Naamini kuna kitu umejifunza kotoka na makala hii. Tafadhali tuandikie maoni yako hapo chini pia usisahau kuwashirikisha wengine makala hii.

No comments:

Powered by Blogger.