Uhuru Kenyatta: Sikubaliani na uamuzi wa Mahakama lakini Ntauheshimu
Rais
wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema kuwa hakubaliani na uamuzi wa Mahakama
ya Juu nchini humo ya kubatilisha uchaguzi wa urais uliopita na kuagiza
kufanyika upya kwa uchaguzi lakini anaheshimu uamuzi huo wa mahakama.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo kuhusu uamuzi huo wa Mahakama, Rais
Kenyatta amesema kuwa Jubilee iko tayari kurejea kwenye uchaguzi kama
Mahakama ilivyoamuru huku akiwataka Wakenya kudumisha amani.
“Wenzangu,
amani… amani… amani. Mshike jirani yako mkono umwambie hii ni vita ya
wale, sisi ni kitu kimoja. Sisi ni jamii ambayo inaitwa ‘Wakenya’ na
hivyo ndivyo itakavyokuwa,” amesema Kenyatta.
“Na mimi namshukuru ndugu yangu hapa [Ruto] amesema yuko tayari kurudi uwanjani,” ameongeza.
Kenyatta
amewataka Wakenya kujiandaa na uchaguzi mwingine na kwamba Jubilee
wataingia tena barabarani ‘kupiga debe’ ili wachaguliwe tena.
Leo,
Mahakama ya Juu iliamua kubatilisha uchaguzi wa Rais uliofanyika Agosti
8 mwaka huu ambao kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo,
Kenyatta alishinda kwa zaidi ya asilimia 54 dhidi ya Raila Odinga (NASA)
aliyepata asilimia 44.7.
Mahakama
imeeleza kuwa kulikuwa na vitendo vya ukiukwaji wa sheria na katiba ya
nchi hiyo uliopelekea uchaguzi huo kutofaa kuwa halali. Imeamuru
uchaguzi huo kufanyika baada ya siku 60 (Novemba Mosi).
No comments:
Post a Comment