Lissu ampa ujumbe mzito Zitto, "Tumeshinda"
Lissu ampa ujumbe mzito Zitto, ‘Tumeshinda’
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameeleza ujumbe aliopewa na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alipomtembelea katika hospitali ya Nairobi anapopatiwa matibabu kufuatia tukio la kushambuliwa kwa risasi mwanzoni mwa mwezi huu.
Zitto ambaye ni Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, amesema kuwa ujumbe aliopewa na Lissu umempa ujasiri zaidi na kumponya moyo wake ingawa yuko katika maumivu makali.
“Nilitumia wikendi yangu kuwa na Lissu jijini Nairobi. Nimerudi hakika nikiwa mnyenyekevu kutokana na ujasiri ambao ndugu yangu alinionesha,” Zitto ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.
“Kwa maneno tu, washambuliaji wake walimuumiza. Walimuumiza kweli. Lakini bado katika kipindi ambacho nimekaa naye amenionesha ucheshi, ari na shukurani. Huo ni ujasiri,” ameongeza.
Zitto ameeleza kuwa angevunjika moyo zaidi kama Lissu asingemwambia neno zito la ujasiri kuonesha hali ya ushindi ingawa yuko kwenye maumivu makali.
“Analichopitia na anachoendelea kukipitia sio kitu rahisi kwa mtu yeyote. Ninafikiria ingeniacha mnyonge wa moyo, kama sio maneno yake aliyoniambia: “Tumeshinda. Tumeshinda”. Lissu ni jasiri,” ameandika mbunge huyo.
Zitto amewahi kulalamika kuwa yeye pia anatajwa katika orodha inayodaiwa kuwa ya wabunge ambao wanafuatiliwa na ‘watu wasiojulikana’.
Lissu anaendelea kupata matibabu katika hospitali ya Nairobi kufuatia tukio la kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana, lakini kati ya hizo, risasi tano zilimpata.
No comments:
Post a Comment