Alichokisema Raila Odinga Baada ya Mahakama ya Juu Kufuta Matokeo yaa Uchaguzi Kenya
Mgombea
urais wa Kenya kupitia Muungano wa Nasa, Raila Odinga amesema Tume Huru
ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni lazima ifanyiwe mabadiliko ili kurudia
uchaguzi.
Mahakama
ya Juu ya Kenya leo Septemba Mosi imefuta matokeo ya urais yaliyompa
ushindi Rais Uhuru Kenyatta kuwa madarakani kwa muhula wa pili.
Kwa
uamuzi uliotolewa na mahakama, uchaguzi mwingine unapaswa kufanyika
katika kipindi cha siku 60. Iwapo ushindi wa Kenyatta ungeidhinishwa
angeapishwa Septemba 12.
Odinga amesema ni lazima waliosababisha dosari kwenye uchaguzi wa Agosti 8 waondolewe.
“Tume
ya uchaguzi ni lazima isafishwe ili turejee kwenye uchaguzi mwingine na
nina uhakika tutashinda,” amesema Odinga katika mkutano na waandishi wa
habari ambao pia uliwashirikisha viongozi wengine wakuu wa Nasa.
Amesema ni lazima viongozi waliohusika wawajibishwe akisisitiza mitambo ya Tume ya Uchaguzi ni lazima iwe wazi kwa ukaguzi.
Odinga amesema hawana imani na IEBC inayoongozwa na Wafula Chebukati kwa kuwa haikuwatendea haki kwenye uchaguzi huo.
“Leo tunasherehekea sikukuu ya Eid lakini tuna sherehe nyingine ambayo Mahakama imetupatia tunaisherehekea,” amesema.
Amesema
uamuzi wa Mahakama umeipa heshima Kenya katika ujenzi wa demokrasia.
Ameipongeza kwa umakini uliozingatia uamuzi wa Wakenya wa kutaka
uchaguzi huru na wa haki.
“Uamuzi
wa Mahakama umetoa sura mpya na umetuma ujumbe kwa Afrika namna
demokrasia yetu ilivyokomaa. Kulikuwa hakuna haja ya kurudia uchaguzi
kama tume ingeonyesha matokeo katika mitambo yake,” amesema.
Odinga amesema majaji wameonyesha Mahakama zinaweza kuwa na uhuru na kusimama dhidi ya nguvu za marais Afrika.
“Mahakama
imeashiria mwanzo wa Kenya mpya na daima ni kwamba, ukweli ndiyo msingi
wa yote na jina na Jaji Maranga litaendelea kukumbukwa katika historia
ya Kenya,” amesema. David Maranga ndiye Jaji Mkuu wa Kenya.
No comments:
Post a Comment