MKEMIA: MKOJO WA AGNES MASOGANGE ULIKUWA NA HEROIN
Mkemia
kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias Mulima, ameiambia
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa sampuli ya mkojo wa msanii Agnes
Gerald maarufu kama Deal ama Masogange (28) umebainika kuwa na dawa ya
kulevya aina ya heroin.
Akitoa
ushahidi leo Jumatano mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri,
shahidi huyo wa kwanza wa upande wa mashtaka, akiongozwa na Wakili wa
Serikali, Constantine Kakula, ameiambia mahakama kuwa mnamo February 15,
2017 askari wawili kutoka Jeshi la Polisi Tanzania, Koplo Sospeter na
WP Judith, walimfikisha Masogange ofisini kwake kwa lengo la kumfanyia
vipimo vya mjono wake.
Alisema
baada ya kuwapokea, alimsajili Masogange na kumpa namba ya maabara 446
/2017 na kisha kuwakabidhi kifaa maalum kwa ajili ya kuweka sampuli ya
mkojo.
Alidai
baada ya kupokea sampuli ya mkojo ya Masogange alifanyiwa uchunguzi kwa
kutumia kemikali na kubaini kuwa mkojo wake una chembechembe za dawa za
kulevya aina ya heroin ambazo kwa kitaalamu zinajulikana kama Diacety
Imophine.
Aidha, alisema uchunguzi zaidi ulibaini chembechembe za dawa nyingine ya kulevya aina ya Oxazepam.
Shahidi
huyo alidai baada ya kufanya uchunguzi huo, aliandaa taarifa ya
uchunguzi kuhusiana na sampuli hiyo ya mkojo ambapo aliisaini yeye
mwenyewe na kuthibitishwa na kaimu mkemia mkuu wa serikali.
Shahidi huyo alimtambua Masogange kwa ndiye aliyepelekwa kuchukuliwa sampuli hiyo ya mkojo ofisini kwake.
Pia
alidai anaweza kuitambua taarifa hiyo ya uchunguzi kutokana na kuwepo
kwa saini yake, muhuri wa moto wa maabara ya mkemia mkuu wa serikali.
Pia ameomba mahakama kupokea vitu hivyo kama kielelezo cha ushahidi
katika kesi hiyo.
Hata
hivyo, mawakili Nehemiah Nkoko na Reuben Simwanza ambao wanamtetea
Masogange wamepinga taarifa hiyo ya uchunguzi wakitaka isipokelewe na
mahakama kwa madai haijakidhi vigezo vya sheria.
Nkoko
amedai utaratibu wa kisheria haukufatwa kabla ya mtuhumiwa aliyeko
chini ya polisi kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu, kwa kuwa ofisa wa
polisi alitakiwa kuwasilisha maombi mahakamani ndipo amri ya kupimwa
itolewe.
Amesema katika ushahidi wake mkemia huyo hajaeleza kama ofisa wa polisi alipeleka amri ya mahakama kutoka mahakama yoyote ile.
"Ripoti
ipo kinyume na sheria, mahakama ina njia moja tu nayo ni kuikataa na
sio kuikubali. Sheria ipo wazi, tunaomba mahakama ikubali pingamizi letu
na kukataa kupokea taarifa hiyo," alisema.
Naye
Wakili Simwanza alidai ripoti hiyo ikitazamwa inataja fomu nyingine ya
ombi la Jeshi la Polisi kwenda kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya kufanya
vipimo.
Amedai
ripoti hiyo ipo yenyewe bila ya kuambatanishwa na fomu maalum
inayotumiwa na polisi kupeleka sampuli hivyo haiwezi kupokelewa na
kutumika kama kielelezo.
Akijibu hoja hizo, Wakili Kakula alidai mapingamizi hayo hayana mashiko wala miguu ya kusimamia.
Amedai
fomu ambayo haijaambatanishwa na ile ya mkemia mkuu ni vitu viwili
tofauti na hata uwasilishwaji wake unafanywa na watu wawili tofauti.
Alisema taarifa ya mkemia inawasilishwa na mkemia na ile ya polisi inawasilishwa na polisi.
Kuhusu
hoja ya sampuli ya mkojo, Kakula alidai kifungu cha 63 cha Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kimeweka mazingira ambayo ofisa wa
polisi atawasilisha maombi mahakamani kuweza kuchukua sampuli.
Alisema iwapo mtuhumiwa anakataa kuchukuliwa sampuli ya mkojo, hivyo atawasilisha ombi mahakamani ili iweze kutolewa amri.
Kakula
alisema katika pingamizi lao upande wa utetezi haijaeleza kwamba
mshitakiwa alikataa kupima, akalazimishwa. Aliomba mapingamizi hayo
yatupiliwe mbali.
Hakimu
Mashauri ameahirisha shauri hilo hadi Agosti 28, 2017 kwa ajili ya
kutoa uamuzi wa ama kupokelewa kwa taarifa hiyo ama la.
Masogange
amefikishwa mahakamani hapo akidaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya
heroin kati ya Februari 7 na 14, mwaka huu, katika maeneo yasiyojulikana
ndani ya jijini a Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment