Gigy Money Unaanzaje Kumponda Stara Thomas?
Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema wake wa kuniwezesha kukutana nanyi kwa mara nyingine katika safu yetu hii yenye lengo la kuwekana sawa, hasa kwa vijana wetu mastaa wa fani mbalimbali.
Wiki hii kuna mambo mengi yametokea katika jamii yetu, ikiwemo kuingia kwa wimbo mpya wa msanii wa Hip Hop, Roma Mkatoliki iitwayo Zimbabwe ambayo imepokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki pamoja na watu wa kada mbalimbali.
Sikuwahi kuwa na wazo la kuandika barua kwa mdogo wangu Gigy Money kwa sasa, lakini kutokana na kilichotokea nimelazimika kumuandikia barua, kwanza kwa ajili ya kumkumbusha asichokijua halafu kwa lengo la kumfunda, kama msanii kinda!
Malkia wa muziki wa Zouk nchini, Stara Thomas alihojiwa na chombo kimoja cha habari na kutoa maoni yake juu ya kuwepo kwa nyimbo nyingi zinazoimbwa siku hizi ambazo hazina maadili, akisema jambo kama hilo linachangiwa pia wakati mwingine na malezi ambayo msanii husika amepitia.
Lakini kana kwamba maneno hayo yalikuwa yamesemwa kwa ajili ya muuza sura kwenye video za wasanii wa Bongo Fleva, Gigy Money akapandwa na povu kubwa, akaibuka na kumponda Stara, kwamba licha ya kuwa hajui alichokisema, lakini pia hakuwa akiimba chochote zaidi ya ngonjera!
Sina uhakika na umri wa Gigy Money, lakini kwa vyovyote atakuwa ni binti mdogo ambaye hataki kuifahamu historia ya kitu kinachompa maisha hapa mjini. Yes, huyu anaendesha maisha yake kupitia muziki, kama siyo kuuza sura katika video za wenzake, basi wakati mwingine hujaribu mwenyewe kuimba.
Tatizo siyo kumjibu Stara, bali namna alivyojaribu kuwasilisha hayo maoni yake, ni kama vile mwimbaji huyo mkongwe si lolote si chochote, kitu ambacho siyo sawa kabisa.
Kwa kumsaidia Gigy na chipukizi wenzake wanaotaka kuufanya muziki, ni vyema wakatambua historia ya kitu wanachokipigania. Kama angefanya hivyo, asingethubutu kumwambia Stara kuwa alikuwa anaimba ngonjera.
Au inawezekana pia kwa maoni yake, nyimbo za Stara ni kama ngonjera, lakini vizuri pia kutambua kuwa kila enzi zina mitume wake, hivyo siyo sahihi kuwaponda mitume wa enzi za kale za mawe kwa sababu hivi sasa tupo katika zama za dotcom!
Ilikuwa ni lazima wawepo akina Stara Thomas katika kutengeneza mazingira ambayo sasa yanamruhusu Gigy Money na wenzake akina Amber Lulu nao kutamani kuufanya muziki. Hawa ni dada na mama katika muziki huu wa kizazi kipya ambao wanatakiwa kupewa heshima inayostahili.
Hata kama siyo malezi mabaya yanayosababisha kuwepo kwa tungo za ajabu, lakini katika uhalisia kamili, Gigy huna kipaji cha kufanya muziki wa kuweza kumbeza Stara Thomas mbele ya kadamnasi.
Katika Bongo Fleva, Stara ni gwiji. Amefanya muziki ambao unabakia kuwa alama. Ni jambo linalokera kidogo, kukuta watu ambao wanahitaji msaada, ukiwemo wa kisaikolojia ili kuwafanya wawe wanamuziki, leo wanasimama kwa kujiamini na kuwaponda watu ambao tasnia inajivunia.
Stara hakumtaja mtu jina kwa sababu katika ukweli, Gigy siyo mwanamuziki, ni binti mdogo anayetamani kuwa msanii, ndiyo maana hana uhakika na njia anayopita. Leo atafanya kituko hiki, kesho kile ili mradi watu waendelee kumuona, kitu ambacho yeye kwa bahati mbaya, anaamini kitamfanya kuwa mwanamuziki mkubwa.
Kwa aina ya muziki ambao Gigy anaufanya, itamchukua miaka mingi kuweza kuwa na kazi zinazokaribia walau robo ya uzuri katika utunzi, midundo, sauti na mpangilio kwa jumla, achilia mbali heshima mbele ya hadhira.
Ili kumsaidia Gigy ni vizuri kumfahamisha kuwa wapinzani wa Stara kimuziki enzi zake walikuwa ni akina Lady Jaydee, Unique Sisters na Ray C, ambao usingeweza kuwakuta katika kashfa za kijinga kama za kupiga picha za utupu na kuzitupia katika mitandao.
Kuna watu wengine ukiwaponda, ni kama unajiponda mwenyewe, sasa kwa Gigy kusema Stara alikuwa anaimba ngonjera, yeye anaimba nini jamani?
Inawezekana hiyo ndiyo staili yako ya maisha ya kulipuka kwa kila jambo, lakini kwa wenye akili zao, wanazidi kukushusha kwa jinsi unavyokosa heshima kwa watu ambao walitumia muda mwingi, kwa taabu nyingi, tena wakikabiliwa na changamoto nyingi kuufanya huu muziki kuwa ajira kama nyinyi mlivyoukuta.
No comments:
Post a Comment