Waliokata rufaa ya vyeti feki waelekezwa pakwenda
WIZARA ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, imewataka watumishi waliotajwa katika sakata la vyeti feki
vya kidato cha nne, sita na ualimu, kuwasiliana na waajiri wao ili
wapewe matokeo ya hatima ya rufaa zao.
Kauli hiyo imetolewa baada ya kuwapo kwa orodha ya majina ya uongo
yanayosambaa katika mitandao ya kijamii, yanayodaiwa kutolewa na wizara
hiyo, kwamba ni rufaa za wenye vyeti feki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam
jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo,
Florence Temba, watumishi hao waliowasilisha rufaa za vyeti vyao katika
Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), wanapaswa kufuatilia uhalali wa
vyeti hivyo kwa waajiri na si katika mitandao.
“Ipo taarifa inayosambaa katika mitandao mbalimbali, ikiwa na majina ya
wanaodaiwa kuwa ni watumishi wa umma na maeneo yao, na kinachodaiwa ni
matokeo ya rufaa zilizokatwa kuhusu uhalali wa vyeti vya elimu kwa
wahusika,” ilisema taarifa ya wizara.
Pia ilisema taarifa inayosambaa mitandaoni haijatolewa na Serikali na ipuuzwe.
Kwamba watumishi wa umma na wananchi wote wanaelekezwa kuwa Serikali ina utaratibu rasmi wa kutoa taarifa na mawasiliano.
Aprili 28, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alimkabidhi Rais Dk.
John Magufuli majina 9,932 ya watumishi wanaodaiwa kuwa na vyeti feki.
Baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Magufuli, aliagiza watumishi hao
kuondoka wenyewe kazini hadi ifikapo Mei 15, mwaka huu na wasipofanya
hivyo watafikishwa mahakamani.
Pia Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Laurean Ndumbaro, aliwahi kunukuliwa
na gazeti hili akisema idadi ya watumishi waliokata rufaa Necta ni
ndogo.
Alisisitiza kuwa watumishi wengi waliokata rufaa ni wale waliobadili
majina baada ya kaolewa na kuanza kutumia la mume, lakini hakuwasilisha
vyeti vya ndoa.
Alisema kundi hilo na wengine kwa wakati huo walifanikiwa kuhakiki na
kuendelea na kazi, lakini wengi waliohakikiwa walikuwa na vyeti feki.
Ndumbaro alisema uhakiki wa rufaa hizo umesababisha kukwamisha kutolewa
kwa awamu ya pili ya watumishi wenye vyeti feki kwa taasisi na wizara
zake zilizobaki.
No comments:
Post a Comment