Uchaguzi mkuu TFF wasimamishwa
Kamati
ya Utendaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) imesimamisha shughuli
zote za uchaguzi kuanzia jana Jumapili hadi Julai 4 ambapo watakaa kikao
cha kamati hiyo na kutoa maamuzi yatakayofikiwa kuhusu mchakato huo.
Sababu kubwa imeelezwa kuwa ni wajumbe wa kamati ya uchaguzi ya TFF kukataa majina ya baadhi ya wagombea kwa sababu binafsi.
Revocatus
Kuuli ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi amesema kutokuwa na
maelewano kumemsababisha achukue uamuzi wa kuuandikia barua Kamati ya
Utendaji akiiomba isitishe mchakato wa uchaguzi (kwakuwa kanuni zilizopo
zinamruhusu kufanya hivyo) japo kumekuwa na taarifa kuwa Bwana Kuuli
alitofautiana na wajumbe wengine wa Kamati ya Uchaguzi kuhusu hatma ya
Rais wa Shirikisho hilo, Jamal Malinzi ambaye alichukua fomu kutaka
kutetea kiti chake.
Mgogoro
uliosababisha kutoelewana huku umetokana na wajumbe wanne kati ya
watano kutaka jina la Rais wa sasa, Jamal Malinzi, lipitishwe bila
kuwapo – jambo ambalo Revocatus Kuuli anasema si sahihi kikanuni.
Kamati
ya Uchaguzi ya TFF ina wajumbe watano. Kwa sababu hiyo, Mwenyekiti wa
Kamati ya Uchaguzi Mkuu wa TFF Revocatus Kuuli akaiandikia barua Kamati
ya Utendaji ya TFF akitaka mchakato mzima wa uchaguzi usimamishwe na
kuangalia kama Sheria za zoezi zima zinazingatiwa.
“Kikao chetu cha leo kimefanyika lakini hakijatoa maamuzi ya matatizo yaliyotokea jana.”
“Mimi
kama Mwenyekiti wa Kamati nimechukua maamuzi ya dhamana niliyonayo.
Nimemuandikia Katibu juu ya dhamira yangu kuangalia upya mwenendo mzima
wa kamati. Wamekubaliana na maombi yangu na wamenipa barua kwamba
wanaona sahihi mchakato mzima usimame mpaka matatizo yaliyotokea
yatakapopelekwa kwenye Kamati ya Utendaji ambayo ndio yenye mamlaka ya
mwisho.”
“Wamesema
wataitisha kikao Julai 4, 2017 (Jumanne ijayo). Matatizo yalikuwa
mengi, kuna watu wamekatakata majina kwa uonevu tu. Taratibu zinataka
kupindishwa kwa sababu ya kutaka kupendelea watu fulani.”
“Mimi
siwezi kuwa sehemu ya kamati ambayo ipo namna hii, kwa hiyo nashukuru
barua yangu imepokelewa na imefanyiwa kazi kama nilivyokuwa nimetaraji.”
Julai
4, 2017 baada ya Kamati ya Utendaji kukaa na kujadili mgogoro huo
uamuzi wa kuendelea au kutoendelea kwa mchakato wa uchaguzi huo
utatolewa.
Kaimu
Katibu Mkuu wa TFF Salum Madadi amesema amekubali ombi la Mwenyekiti wa
Kamati ya Uchaguzi kuhusu kusimamisha mchakato wa uchaguzi wa TFF
kutokana na kutofautiana kwa wajumbe wa kamati hiyo.
Madadi amesema Kamati ya Utendaji ya TFF itakutana Jumanne Julai 4, 2017 kwa ajili ya kulitolea uamuzi suala hilo.
“Kumetokea
mgawanyiko ndani ya kamati yetu ya uchaguzi, Mwenyekiti wa kamati ya
uchaguzi ametuandikia barua na tumeshauriana naye kusitisha mchakato wa
uchaguzi na tumeitisha kikao cha dharura cha kamati ya utendaji ya TFF
tarehe 4 Julai, 2017 saa 7:00 mchana.”
“Baada ya kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji tutakuwa na cha kusema kuhusu mchakato wa uchaguzi,” alisema Madadi.
No comments:
Post a Comment