Trending News>>

Taarifa muhimu kwa watu wanaogombea nafasi za uongozi UVCCM

Demokrasia ni jambo muhimu linalohitajika kuheshimiwa na kuenziwa ndani na nje ya Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa miaka kadhaa kumekuwa na shutuma pia tuhuma zilizokaribia kuotesha mizizi ya kuwepo rushwa ambazo nusra zivunje heshima ya chama chetu na jumuiya zake. Jambo hilo sasa halitaruhusiwa tena wala kuachiwa lifanyike .
Kiongozi wa UVCCM mahali popote atachaguliwa baada ya kufanyika chaguzi huru na za haki, kuzingatia Kanuni na Taratibu za Uchaguzi kama zilivyoagizwa na vikao husika bila ya kukiuka, kupuuzwa au kuvunjwa.
Nia ya UVCCM ni kujenga haiba mpya na njema ya kuheshimu misingi ya demokraia ya kweli, kuwa na adabu na kufuata nidhamu, miiko na maadili kwa kila anayetaka kuchagua au kuchaguliwa.
Jana Jumapili tarehe 02/07/2017 zoezi la utoaji fomu kwa Waombaji wa nafasi mbali mbali za Uongozi katika Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM lilianza rasmi ngazi ya Wilaya, Mikoa na Taifa.
Kwa Ngazi ya Taifa nafasi zote fomu zinatolewa Dodoma ghorofa ya 3 chumba Na. 45, Ofisi Ndogo za UVCCM Dar es Salaam ghorofa ya 7 na Afisi Kuu ya UVCCM Gymkana Zanzibar.
Fomu zote zirejeshwe si zaidi ya tarehe 10/07/2017 Saa 10.00 Jioni katika maeneo yaliyoainishwa.
Ifahamike kuwa kila Kijana wa Chama Cha Mapinduzi ana haki ya msingi kugombea nafasi yoyote ile kwa mujibu wa Kanuni ya UVCCM na katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kama iliyo Haki na Wajibu wa mwanachama kugombea, kuchagua au kuchaguliwa, ndivyo inayostahili mwanachama kufuata taratibu na kuheshimu kanuni pamoja na taratibu za uchaguzi.
UVCCM imekusudia kurudisha nidhamu ya Chama hasa katika suala zima la kugombea nafasi za uongozi na haki ya kuchagua au kuchaguliwa.
Muomba nafasi anayo haki ya kutia nia, kuchukua fomu ya kuwania Uongozi bila ya kufanya mbwembwe, shengesha au mikogo ambayo kwa namna moja au nyingine itaonyesha hali ya kujinadi mapema, kujitangaza na kufanya kampeni.
Muomba nafasi yoyote ajaze fomu zake kwa uangalifu, azingatie tarehe na siku ya kurudisha mahali husika tena kwa kujali wakati uliopangwa kikanuni na kuheshimu taratibu.
Sifa au wasifu wa kila muomba nafasi kwa kadri atakavyojaza fomu yake utajielekeza na kuandikwa kama ilivyo katika kitabu maalum cha wagombea wote ambacho kitasomwa na wajumbe wapiga kura siku ya uchaguzi husika hivyo ni vyema kuwa makini na taarifa zako.
Ni marufuku na hatakiwi kabisa muomba nafasi yoyote ile Mara baada kuchukua au kurejesha fomu kuandika bango au kipepeprushi na kuvigawa, kuvieneza au kuwatuma wapambe wake wakati taratibu nyengine za vikao bado hazijakamilika.
Kila muomba nafasi atapata nafasi ya kujieleza, kutoa wasifu wake, kutaja dhamira na malengo yake mbele ya wajumbe wa Mkutano husika wa kuchaguliwa si kinyume na hivyo baada ya taratibu za Vikao kukamilika.
Kuanza mapema kampeni au wapambe kufanya ushabiki wa kisiasa na kumnadi, kumpiiga debe pia kwenda katika vyombo vya habari na kueleza wasifu, sifa au kutaja nafasi anayogombea na kujinadi kutahesabika ni kufanya kampeni mapema na kumfanya apoteze sifa.
Ni marufuku na haitaruhusiwa kabisa muda ukifika kwa mgombea yeyote kufanya kampeni za kihuni kwa kutumia lugha chafu, siasa za maji taka, matusi, dharau kinyume na ubinadamu pia kushiriki kejeli dhidi ya wenzake.
Muomba nafasi katika ngazi yeyote ambaye hatazingatia wala kuheshimu na kutofuata maelekezo haya anaweza kujipotezea sifa ya kuteuliwa na kushiriki kwake katika chaguzi huru na za kidemokrasia ndani ya UVCCM.

No comments:

Powered by Blogger.