Mara nyingi nilikuwa nikimshauri sana Sara, kuachana na mpenzi wake
kutokana na mpenzi wake huyo kuwa na tabia mbaya. Ambapo wakati mwingine
alikuwa akimpiga sana. Siku hiyo nilikuwa nyumbani nimepumzika ghafla
nilisikia mlangoni kuna mtu anabisaha hodi kwa nguvu. "Suzi, Suzi,
naomba ufungue mlango John ananiuwa" Ilikuwa ni sauti ya Sara
nilinyanyuka haraka na kufungua mlango Sara alionekana kuumia maeneo ya
usoni nilishtuka sana kumuona katika hali ile "Hee! Umepatwa na nini
Sara, mbona hivyo kulikoni?" Nilimuuuliza huku nikimkaribisha ndani.
Aliingia na kuketi lakini bado alikuwa analia kwa uchungu huku akisema
"Yaani mimi kweli John ni wakunifanyia hivi, wakati nimemfumania na
mwanamke mwingine? Halafu ananipiga" Nilisogea na kuketi karibu huku
niki mliwaza "Pole sana Sara, lakini kwanini anakupiga, kwa kosa lipi
ulilomfanyia, huyu mwanaume ana kichaa heee! na wewe rafiki yangu
mwanaume kama huyo hakufai ni bora uachane naye kabisa. Embu tizama
umemfumania halafu anakupiga, usiwe mjinga kiasi hicho Sara wanaume
wapo wengi, kama yeye anakuona wa nini, basi ajue kuna wengine
wanafikiria watakupata lini. Mwanaume gani mshamba huyo usipoangalia ipo
siku atakuvunja mguu".
Niliongea maneno mengi huku nikimtizama Sara aliyekuwa anaendelea kulia
akasema "Inaniuma sana, kwa jinsi ninavyompenda John, lakini sasa
siwezi kuendelea kuwa naye bora tuachane kabisa". Na mimi nilikuwa
namshauri asikubali kuendelea kuwa na uhusiano na John kutokana na
ukatili anaomfanyia.
Tuliendelea kuzungumza huku nikimliwaza Sara, ilifika majira ya saa
mbili usiku nikiwa naandaa chakula, huku Sara akiwa ameketi sebuleni
mara mlango ulifunguliwa kwa nguvu, na aliyekuwa amekuja muda huo
alikuwa ni John, nilisogea na kuongea kwa sauti ya jazba "Umefuata nini
hapa kwangu, naomba utoke nje, mwanaume muuaji wewe.Toka nje John sitaki
kukukona hapa kwangu" Sara alikuwa ameketi huku akiwa amejiinamia bila
ya kuzungumza chochote.
John alinitizama na kusema "Nimekuja kumchukua mpenzi wangu" Alisema
John kwa kujiamini, nilicheka kwa dharau na kusema " Unanichekesha kweli
wewe, eti nimekuja kumchukua mpenzi wangu, kama unampenda kweli kwanini
unamsaliti na tena kama haitoshi unampiga" John hakunijibu chochote
alimsogeleaa Sara na kumshika mkono "Darling (mpenzi) nakuomba twende
nyumbani tukazungumze, nakupenda sana Sara"
Niliwatizama ilikuona Sara atasemaje lakini hakuongea chochote na
baadaye aliinuka na kuondoka na John bila hata ya kula chakula
nilichokuwa nimeandaa, nilibaki nashangaa na kuzungumza na nafsi yangu
"Makubwa haya, inamaana huyu Sara na kuumizwa kote huko bado anaondoka
na John ama kweli mapenzi ni kipofu".
Zilipita takribani kama wiki mbili tokea Sara aje nyumbani kwangu. Siku
hiyo nilikuwa katika mizunguko yangu ya hapa na pale maeneo ya kariakoo.
Nikawa nimeingia katika duka moja la nguo, nilimkuta John mchumba wake
na Sara nilimsalimia lakini hakuitikia alinyamaza kimya, na mimi
sikumjali, mara ghafla katika chumba kidogo cha kujaribishia nguo
alitoka mwanamke huku akiwa anazungumza na John " Mpenzi nimependeza,
asante sana asali wa moyo wangu hii nguo ni nzuri nimeipenda" Yule
mwanamke alikuwa akijishebedua huku akimshikashika John mikononi. Wakati
wote huo nilikuwa nashangaa nikiwa siamini nianachokiona, lakini
ilinibidi nikae kimya.
Bila ya aibu wala wasiwasi John alimnunulia nguo nyingi yule dada na
waliondoka na mimi nilinunua nguo niliyoipenda na kuondoka.
Nikiwa nyumbani kwangu niliwaza na kumuonea huruma sana Sara ambaye
alikuwa anampenda John kwa moyo wake wote, Nilifikiria na kuamua ni bora
nimweleze Sara kile nilichokiona "Yaani hawa wanaume sijui wako vipi
jamani, Sara ni mwanamke mrembo sana kuliko hata yule mwanamke ambaye
John alikuwa naye pale dukani, hili jambo siwezi kukaa nalo moyoni ngoja
nimpigie simu rafiki yangu nimweleze". Basi nikachukua simu yangu na
kumpigia Sara nikamsimulia kila kitu nilichokiona Sara alisikitika na
kusema "Jamani kweli John ananifanyia hivi, mimi nimemkosea nini huyu
mwanaume au kwasababu nampenda, asante sana Suzi kwa kunipa taarifa huyu
mwanaume ni bora niachane naye" Na mimi kwa msisitizo nikamshauri "Ni
bora kabisa uachane naye, mbona wanaume wapo wengi huyo wanini mwanaume
ambaye kila mwanamke atakayepita mbele yake anamtamani, rafiki yangu
huyo mwanaume hakupendi" Tuliendelea kuongea na baadaye kila mtu
aliendelea na kazi zake.
Baada ya miezi miwili tokea nizungumze na Sara sikuhiyo alikuja rafiki
yangu anaitwa Maria nilifurahi sana kwani tulikuwa hatujaonana muda
mrefu. Maria alikuja na kuniletea kadi ya mchango wa harusi "Rafiki
nimepita hapa kwako mara moja kukuletea kadi ya mchango wa harusi ya
Sara na John wameamua kufunga pingu za maisha" Nilishtuka na kusema "Eti
unasema Sara na John kwani si walikuwa wameachana?" Niliuliza kwa
umakini "Mmmh wewe Suzi acha hizo, ila mimi nimepata fununu kuwa wewe
ndiyo ulikuwa unawachonganisha, na tena ulikuwa unamtaka John kimapenzi
ndiyo maana ulikuwa unataka watengane." Alisema Maria huku akinitizama,
mimi nilikuwa nimepigwa na butwaa na kusema "Jamani mimi, nilikuwa
nawachonganisha? Nani anazusha maneno hayo ya uongo, hata siku moja
sijawahi kuwaza kumtaka kimapenzi huyo John, ama kweli binadamu wabaya,
leo hii Sara ananiona mimi nilikuwa namchonganisha?" Nilibaki nashangaa
na Maria aliondoka na kuniacha peke yangu. Siku hiyo nilijisikia vibaya
sana lakini pia nikawa nimejifunza jambo. Tokea siku hiyo nilikuwa
sipendi kabisa kutoa ushauri katika suala la mapenzi baina ya wawili
wapendanao. Nimeamua BORA KUKAA KIMYA. Kwani unaweza kutoa ushauri ukiwa
na lengo zuri lakini ukaonekana mbaya. NI BORA KUKAA KIMYA.
No comments:
Post a Comment